Habari Mseto

Tullow kuanza kuchimba mafuta baada ya kupata idhini ya NEMA

May 5th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

KAMPUNI ya mafuta, Tullow itaanza kuchimba mafuta kwa kiwango kidogo eneo la Lokichar Kusini kuanzia wiki hii.

Kampuni hiyo itachukua hatua hiyo baada ya kupokea idhini ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA).

Katibu Mkuu wa Mafuta Andrew Kamau Ijumaa alisema Tullow inatarajiwa kusafirisha takriban mapipa 2,000 ya mafuta kila siku.

Kutokana na hilo, Kenya itakuwa katika mkondo wa mataifa yanayouza mafuta ulimwenguni.

Mzigo wa kwanza wa mafuta utasafirishwa kuanzia Juni, kabla ya uchimbaji kamili wa mafuta nchini kuanzia 2022.

Kufikia sasa, Bw Kamau alisema zaidi ya mapipa 80,000 ya mafuta yamesafirishwa kutoka Lokichar hadi Bandarini Mombasa na yanangoja kuuzwa.

Mapipa 200,000 ya kwanza yatauzwa kwa kampuni ya kusafisha mafuta itakayotoa bei ya juu, alisema Bw Kamau.

Hata hivyo, alisema kuwa bado ni mapema kutambulisha wanunuzi. Maafisa wa Tullow na serikali walianza kukutana Machi kutafuta wanunuzi.

Kulingana na Kamau, wanunuzi kufikia 18 wa kimataifa kutoka China, Ulaya na kwingineko walionekana kuwa na azimio la kununua bidhaa hiyo. Alisema kampuni hizo zitazingatiwa wakati wa utoaji wa tenda katika soko wazi la kimataifa.

Pipa moja litauzwa kwa dola 50 kulingana na maafikiano, alisema katibu huyo. Kenya itakuwa ikitathmini masoko ya kimataifa kabla ya muda rasmi wa kuanza kuchimba na kuuza mafuta 2022.