Tumaini la wadau wa utalii liko kwa serikali

Tumaini la wadau wa utalii liko kwa serikali

NA SIAGO CECE

WADAU katika sekta ya utalii Pwani wana matarajio kuwa serikali mpya ya kitaifa na za kaunti zitatatua kilio chao cha miaka mingi kuhusu hitaji la ndege za kimataifa kuruhusiwa kusafiri moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa Moi, mjini Mombasa.

Hii ni baada ya Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, kuahidi kuwasilisha suala hilo mbele ya Baraza la Magavana ili kushinikiza serikali ya kitaifa iitikie wito huo.

Kwa sasa watalii wengi wanaoelekea Pwani kutoka nchi za kigeni hulazimika kutua Nairobi kwanza. Akiongea afisini mwake baada ya kukutana na wadau kutoka Chama cha Utalii wa Pwani za Kenya (KCTA), Bi Achani alisema utekelezaji wa wito huo ni muhimu kwa uchumi wa Kwale na Pwani kwa jumla.

Alisema atashinikiza suala hilo litiliwe mkazo pia na magavana wenzake wa Pwani kupitia Jumuiya ya Kaunti za Pwani.

“Tuna vivutio bora zaidi, hasa ufuo wa Diani hapa Kwale ambao umeshinda tuzo nyingi duniani. Lakini changamoto zinazojitokeza wakati wa kusafiri kwa kushukia miji mingine kabla ya kufika Mombasa, watalii huwa wanachagua maeneo mengine ya kuenda,” akasema.

Mwenyekiti wa KCTA, Bw Victor Shitakha, alisema hatua ya Bi Achani ikifua dafu itapiga jeki sekta ya utalii Pwani.

“Tuna matumaini kuwa Bi Achani atashughulikia masuala ambayo ambayo ameahidi. Kama chama, tuko tayari kushirikiana kwa njia yoyote iwezekanayo,” Bw Shitakha akasema.

Wakazi wengi wa Pwani hutegemea watalii kwenye biashara zao lakini biashara nyingi zimetatizika kwa miaka mingi sasa tangu sekta hiyo ilipoanza kufifia.

  • Tags

You can share this post!

NPSC yateua kaimu DCI kushikilia kazi ya George Kinoti...

Katungwa aendelea kuhangaisha mabeki soka ya wanawake India

T L