Michezo

Tumaini tuzo ya Mwanariadha wa Bora wa Mwaka Duniani kwa upande wa wanawake itatua Kenya kwa mara ya kwanza 2020

November 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUJUMUISHWA kwa Faith Kipyegon, Hellen Obiri na Peres Jepchirchir kwenye orodha ya watimkaji wanaowania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka wa 2020 kunawapa Wakenya tumaini kwamba tuzo hiyo itatua humu nchini kwa mara ya kwanza mshindi atakapotangazwa rasmi mnamo Disemba 5.

Licha ya baadhi ya wanariadha wa Kenya kutikisa dunia katika fani mbalimbali za mbio za masafa ya kadri na marefu, hakuna mwanamke ambaye amewahi kujitwalia tuzo ya Mwanariadha Bora wa Mwaka.

Hafla ya kutolewa kwa tuzo za mwaka huu itaandaliwa na Shirikisho la Riadha Duniani (WR) kupitia mtandao kwa sababu ya janga la corona.

Licha ya kalenda ya mashindano mengi kutatizwa na Covid-19, Obiri alijivunia msimu wa kuridhisha mwaka huu. Bingwa huyu wa dunia katika mbio za mita 5,000 hakuzidiwa maarifa katika mapambano matatu ya mita 3,000 na mita 5,000 kwenye kipute cha Diamond League na aliweka muda bora wa dunia wa dakika 8:22.54 kwenye duru ya Doha, Qatar mnamo Septemba 25.

Kwa upande wake, Jepchirchir alivunja rekodi ya mbio za kilomita 21 duniani kwa wanawake mara mbili kwa kusajili muda wa saa 1:05:34 kisha 1:05:16. Alipata ufanisi huo kwenye Prague Half Marathon na Nusu Marathon ya Dunia nchini Poland.

Kipyegon naye alijivunia mojawapo ya kampeni bora kwenye ulingo wa riadha mwaka huu baada ya kutoshindwa kwenye mashindano matano tofauti huku akisajili muda bora wa dunia wa dakika 1:57.68 kwenye mbio za mita 800 na dakika 2:29.15 kwenye mbio za mita 1,000 katika duru ya Doha Diamond League nchini Qatar.

Japo Wakenya wanapigiwa upatu wa kutwaa taji la wanawake kwa mara ya kwanza mwaka huu, watatu hao watakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Mwingereza Laura Muir, Letesenbet Gidey na Ababel Yeshaneh wa Ethiopia na Sifan Hassan wa Uholanzi.

Mwingine ni malkia wa mbio za masafa mafupi raia wa Jamaica, Elaine Thompson-Herah. Hassan ambaye ni mzawa wa Ethiopia anashikilia anashikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 10,000 na pia ndiye bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500.