Habari Mseto

Tume kuchunguza vifo vya watoto 14 shuleni

February 10th, 2020 2 min read

CHARLES WANYORO na BENSON AMADALA

TUME ya Utendaji Haki kwa Umma, leo imepanga kutembelea Shule ya Msingi ya Kakamega kuchunguza vifo vya wanafunzi 14 walioangamia walipokanyangana wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bi Florence Kajuju anasema watachunguza iwapo afisa yeyote wa serikali alizembea katika wajibu wake.

Akiongea na Taifa Leo, Bi Kajuju alisema watakagua jengo hilo lenye orofa tatu na kuona ikiwa linafaa kutumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi.

Wakati wa upasuaji wa miili uliofanywa Ijumaa wiki iliyopita, baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliokufa walisema hawakuridhishwa na jinsi upasuaji ulivyofanywa.

Bi Kajuju alisema pia wataangalia ikiwa Mamlaka ya Ujenzi wa Kitaifa ilichunguza na kuidhinisha jengo hilo kuwa salama kwa wanafunzi kusomea, na ikiwa tathmini yao iko sawa.

“Tutaangalia ikiwa mipango ilifuatwa, kama kulikuwa na vyuma vya kujishikilia kwa sababu ninaambiwa hakukuwa na vyuma hivyo kati ya mahali ambapo wanafunzi wangeshikilia. Pia tutaangalia jengo hilo kuona kama mpango na muundo ulikuwa kwa kiwango sahihi,” akasema.

Bi Kajuju aliongeza kuwa ikiwa afisa yeyote wa serikali atapatikana na hatia, tume yake inaweza kupendekeza kwamba mkosaji azuiliwe kuwa ofisini yoyote ya umma, aondolewe kutoka ofisi ya umma na kulipia uharibifu huo.

“Kifo cha wanafunzi 14 hakiwezi kuchukuliwa kimzaha. Tutachukua hatua za kisheria,” Bi Kajuju akaonya.

Wanafunzi wawili ambao walikufa kwenye kisa hicho walizikwa Jumamosi.

Nicole Achola, mwanafunzi wa Darasa la tano alizikwa nyumbani kwa wazazi wake mtaani Maraba. Alikuwa katika shule hiyo kwa miaka miwili pekee.

Babake Nicole, Bw Dalmas Khalusi Masayi, akitiririkwa na machozi alielezea jinsi binti yake alivyofanya bidii masomoni na jinsi alivyokuwa mchangamfu.

“Nitampeza binti yangu sana. Alikuwa kipenzi cha watu wengi,” Bw Masayi akanena.

Mamake Nicole alishikwa na huzuni tele kiasi cha kutoweza kuongea na waombolezaji.

Prince Vermaline, 10, mwanafunzi katika darasa la nne alizikwa Khumusalaba katika kaunti ndogo ya Khwisero.

Mamake, Bi Lavender Akosa hakuweza kuzuia machozi yake na kusema kifo kilimpokonya mtoto wake wa pekee.

Wanafunzi wengine wawili, Fidel Kumbutie kutoka Chimoi katika kaunti ndogo ya Kakamega Kaskazini na Samuel Simekha kutoka Bunyore katika Kaunti ya Vihiga walizikwa jana.

Wanafunzi wengine watatu, Antonnet Iramwenya, Venesa Adesa na Simon Waweru watazikwa leo katika kijiji cha Chamakoti katika Kata ya Vihiga, Navakholo, Eshisiru katika Kaunti ya Kakamega na Milima Mitatu eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru.

Wanafunzi wengine, Bertha Munywele, Catherine Aloo na Lavenda Akasa watazikwa Jumamosi ijayo.