NA MARY WANGARI
POLISI sasa huenda wakaanza kuvalia sare zao za zamani tena iwapo Jopokazi Maalum linaloshughulikia mageuzi katika idara ya polisi litaidhinisha mapendekezo yaliyowasilishwa jana Alhamisi na Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC).
Ikiwasilisha mapendekezo yake kwa jopokazi linaloongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, Tume hiyo ya kuajiri polisi ilisema inahitaji kutengewa fedha ili kuwezesha polisi kutengenezewa sare mpya zinazowatosha.Mwenyekiti wa NPSC, Eliud Kinuthia, alisema mchakato wa kuanzisha sare mpya kwa maafisa wote wa polisi mnamo 2018, haukutekelezwa kikamilifu huku akipendekeza “kurejelea sare za zamani kwa majukumu ya kawaida.”
Katika hatua ambayo huenda ikawezesha polisi wa kike kutia mfukoni Sh30,000 zaidi, NPSC inataka maafisa wanaotarajia kujifungua kutengewa fedha za kuwawezesha kununua mavazi ya ujauzito.
“Sare tunazotumia kwa sasa si mwafaka kwa polisi wa kike wenye mimba. Kando na malipo wanayopatiwa katika likizo ya kujifungua, tunapendekeza watengewe pesa za kuwawezesha kununua mavazi ya ujauzito,” ilisema NPSC kupitia ripoti iliyowasilishwa kwa Bw Maraga.
Kuanzishwa kwa Hazina Maalum ya kusaidia familia za maafisa wa polisi wanaoaga dunia wakiwa kazini, vituo zaidi vya kutoa huduma za ushauri nasaha na wa kisaikolojia kwa polisi na kutengwa kwenye bajeti fedha za kuajiri washauri nasaha ni miongoni mwa mapendekezo yaliyowasilishwa katika siku ya nne ya vikao vinavyoendelea katika Bomas of Kenya, Nairobi.
Subscribe our newsletter to stay updated