HabariSiasa

Tumefungiwa Ikulu, wanasiasa wa Rift Valley walia

March 14th, 2019 2 min read

BENSON MATHEKA NA CHARLES WASONGA

SENETA wa Kericho, Aaron Cheruiyot amelalamika kuwa viongozi wa Rift Valley Kusini wameshindwa kumfikia Rais Uhuru Kenyatta, tangu alipoafikiana kufanya kazi na kiongozi wa ODM, Raila Odinga mwaka 2018.

“Ninawaambia kuwa hii ‘handisheki’ inavuruga maendeleo,” akasema Bw Cheruiyot kwenye kipindi cha mjadala katika runinga ya NTV.

“Tumeshindwa kukutana na Rais kama ilivyokuwa kabla ya ‘handisheki’. Sasa inatubidi sisi viongozi wa Rift Valley Kusini kumwandikia Rais barua kuhusu kucheleweshwa kwa ufadhili wa miradi ya maendeleo. Nathibitisha haya kwa sababu nimeweka sahihi barua kama hizo,” akasema Bw Cheruiyot.

Viongozi wa Rift Valley wamekuwa wakilalamika kutengwa nau Rais Kenyatta tangu yeye na Bw Odinga walipoafikiana kushirikiana mwaka jana. Miongoni mwa waliolalamika ni Gavana Stephen Sang wa Nandi, Mbunge wa Kapsaret, Oscar Sudi na mwenzake wa Soy, Caleb Kositany.

“Tungetaka kumkumbusha Rais kuwa Rift Valley tulimpigia kura nyingi zaidi kuliko eneo lingine. Ni kwa nini ametutenga?” Bw Sudi alisema awali.

Viongozi hao pia wamekuwa wakidai kuwa vita dhidi ya ufisadi vina lengo la kukwamisha miradi mikubwa ya maendeleo eneo hilo na kumzuia Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Lakini hapo jana, Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki alikanusha madai hayo akisema haja kuu ni kulinda mali ya umma.

Bw Kariuki, ambaye ni mwenyekiti wa kamati shirikishi inayoendesha vita dhidi ya ufisadi, pia alifafanua kuwa zoezi hilo halilengi watu kutoka jamii au eneo fulani, bali wale wanaoshukiwa kuiba pesa za umma.

“Hatuendesha vita hivi kwa nia ya kutimiza malengo fulani ya kisiasa. Tunafanya kazi hii kitaalamu bila kuendeleza maslahi ya kibinafsi. Lengo letu ni kuzuia wizi wa pesa za umma kwa kuhakikisha kuwa haki imetendeka bila mapendeleo,” Bw Kihara aliambia Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Haki za Kibinadamu.

Alikuwa ameandamana Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) George Kinoti, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbaraki na Mkuu wa kitengo cha kutwaa mali ya ufisadi Muthoni Kimani.

Alisema kuwa kila taasisi inayoshiriki katika juhudi za kupambana na ufisadi inaendesha majukumu yake kwa njia huru bila kuingiliwa kwa njia yoyote.

Akiunga mkono kauli hiyo, Bw Haji alifichua kuwa uchunguzi unaoendelezwa kuhusu malipo ya Sh21 bilioni kwa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, utasambazwa katika miradi katika maeneo mengine ya nchi.

“Baada ya kukamilisha uchunguzi wa sakata ya Arror na Kimwarer tunapanua uchunguzi wetu katika maeneo ya Kati, Mashariki na Pwani,” akasema Bw Haji.