Habari

Tumetumwa na Uhuru kupigia debe ODM Kibra – Kieleweke

October 7th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wa Chama cha Jubilee walio katika kundi la Kieleweke wamewataka wakazi wa eneobunge la Kibra kumpigia kura mwaniaji wa ODM Bernard ‘Imran’ Okoth, huku wakidai kwamba anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Mgombeaji wa Jubilee katika uchaguzi huo mdogo ni Bw McDonald Mariga, ambaye wanasiasa hao wanadai anafadhiliwa na ‘maadui’ wa muafaka baina ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Waliongozwa na wabunge Maina Kamanda (Maalumu), Maoka Maore (Igembe Kaskazini), aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi na mbunge wa zamani wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru.

“Mimi ni mbunge maalumu wa chama cha Jubilee na ninaripoti kwa kiongozi wa chama ambaye ni Rais Kenyatta. Siwezi kufanya jambo lolote linalokinzana na kiongozi wa chama. Mkiona ninampigia debe Bw Imran Okoth, mjue yeye ndiye kipenzi cha Rais Kenyatta,” akasema Bw Kamanda aliyekuwa akizungumza katika Kanisa la PCEA, Parokia ya Kibera.

“Imran ndiye mwaniaji wa watu wanaounga handsheki na Mariga ni mwaniaji wa wanaopinga handsheki. Hiyo ndiyo maana hamtaona Rais Kenyatta akija hapa kupigia debe Bw Mariga kwa sababu roho yake iko kwa Imran,” akaongezea.

Hata hivyo, madai hayo hayangethibitishwa kwa njia huru.

Mariga ajipigia debe

Bw Mariga amekuwa akiendeleza kampeni zake Kibra akisaidiwa na wabunge wa Jubilee walio kwenye mrengo wa ‘Tangatanga’ wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Jumapili alikuwa katika maeneo ya Laini Saba ambapo alizidi kuahidi wakazi kwamba akichaguliwa, ataimarisha biashara za vijana na kina mama, na kushirikisha wakazi katika uongozi wake endapo atashinda katika uchaguzi huo wa Novemba 7.

Kwa mara nyingine, Bw Kamanda alidokeza kuwa huenda kukawa na muungano baina ya chama cha ODM na Jubilee kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2022.

“Mnachoona sasa hapa Kibra ndicho kitashuhudiwa 2022, hakutakuwa na chama cha Jubilee wala ODM 2022,” akasema Bw Kamanda.

Bw Maore alisema handisheki baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga imeleta amani na utulivu nchini hivyo wakazi wa Kibra wasiruhusu watu wachache wanaolenga kuvuruga amani kwa masilahi yao ya kibinafsi. Naye Bw Waweru aliwataka wanasiasa wa Jubilee wanaopinga handisheki kujiandaa kuwa katika upinzani 2022.

Kiti cha ubunge wa Kibra kilisalia wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth aliyeaga dunia Julai.

Uchaguzi Mdogo wa Kibra utafanyika Novemba 7.