Tumieni pesa za refarenda kulisha raia – wabunge

Tumieni pesa za refarenda kulisha raia – wabunge

Na DAVID MWERE

WABUNGE watatu wanaitaka serikali kutenga Sh14 bilioni, inazopanga kutumia kwa kura ya maamuzi kubadilisha katiba ya 2010, kukinga Wakenya milioni nne wa kaunti tano zilizofungwa dhidi ya makali ya janga la Covid-19.

Wabunge hao, Seneta Susan Kihika (Nakuru), Kimani Ichung’wah (Kikuyu) na John Kiarie (Dagoretti Kusini) wanawakilisha kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru ambazo juzi zilitangazwa kuwa Ukanda Ulioathiriwa sana na Ugonjwa (DIZ).

Rais Uhuru Kenyatta alifunga kaunti hizo mnamo Machi 26. Wabunge hao waliozungumza wakiwa Nairobi pia wanataka Sh50 bilioni zitolewe kutoka kwa bajeti za wizara za Ulinzi na Usalama wa Ndani kufadhili upimaji wa Covid 19 na kununua chanjo za kutosha Wakenya wote.

Wabunge hao walisema hatua mpya zilizotangazwa na Rais kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo nchini zimewanyima watu njia za mapato hivyo basi kuathiri hadhi yao pia.

“Tunafahamu hasara inayosababishwa na janga la Covid-19. Hata hivyo, tunamweleza rais wetu kwamba hatua hizi zinatishia heshima ya binamu kwa kuwa familia sasa zinakabiliwa na njaa,” alisema Bi Kihika na kuongeza, “hali ni mbaya mashinani”.

Seneta huyo wa Nakuru alihofia kuwa, kukosa kukabiliana na hali hii haraka kutakuwa sawa na kuchochea hasira na kutamauka miongoni mwa Wakenya, hali ambayo alisema inaweza kuwa hatari.

Alisema kwamba haifai kuweka pesa katika akaunti za wizara za Ulinzi na Usalama wa Ndani “wakati tishio kubwa la usalama na vita ambavyo tunafaa kupigana ni dhidi ya janga”.

“Hatua za haraka na dharura zinafaa kuchukuliwa, na juhudi zote na nguvu zielekezwe kwa hatari inayokumba watu wetu. Upimaji na chanjo kwa watu wa kaunti zilizoathiriwa wakati wa kufungwa ni muhimu,” alisema.

Wabunge hao wanataka familia milioni nne katika kaunti zilizofungwa zipewe Sh3,500 kila moja kutoka kwa Sh14 bilioni zilizotengewa kura ya maamuzi.

Bw Ichung’wah aliitaka serikali kurekebisha bajeti yake iweze kusaidia biashara zilizoathiriwa na kufungwa kwa kaunti hizo kama vile mahoteli, vibanda vya chakula, wahudumu wa masoko ambao huuzia mahoteli bidhaa, baa na sekta ya uchukuzi.

Wabunge hao wanataka serikali kufuta riba kwa watu wanaolipa mikopo, na wapewe afueni ya pesa wanazopaswa kulipa kwa miezi sita.

“Akina baba na mama ambao wiki mbili zilizopita walikuwa wanafanya kazi na kununulia watoto wao chakula sasa wanazama katika mafadhaiko wakitazama watoto wakiteseka na kulala bila chakula,” alisema Bw Ichung’wah.

Mnamo Machi 26, 2021, Rais Kenyatta alitangaza hatua mpya za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo ambapo alifunga kaunti hizo tano.

Muda wa kafyu ya usiku katika kaunti hizo pia ulirefushwa kutoka saa nne usiku hadi saa mbili usiku na kumalizika saa kumi alfajiri.

Mikutano ya kisiasa ilipigwa marufuku na baa katika kaunti zilizoathiriwa zikafungwa.

Hoteli na mikahawa pia ilifungwa isipokuwa kwa wateja wa kununua na kuondoka.

Maeneo ya ibada pia yalifungwa kwa muda usiojulikana.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yanyonga wanyonge

TAHARIRI: Watoto walioacha shule watafutwe