Habari Mseto

'Tumieni Valentino Dei kuzuru hifadhi ya historia'

February 13th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

SHIRIKA la hifadhi za kumbukumbu za taifa (National Archives), limetoa mwito kwa wananchi kutumia Valentino Dei kuzuru majengo yake ili kujua kwa undani historia ya nchi hii.

Akizungumza katika maonyesho ya picha za aliyekuwa Rais wa pili, Daniel arap Moi nje ya jengo hilo, afisa Charles Okumu alisema kuwa jumba hilo linahifadhi historia muhimu ambayo kila Mkenya anafaa kuijua.

Nje ya jengo la Archives, Kaunti ya Nairobi, watu wengi hukutana lakini wasimamizi wanasema hakuna wanaojitolea kujua ni nini kinachohifadhiwa mle ndani ilhali ada inayotozwa ni Sh50 pekee.

“Watu wengi huketi tu nje ya jengo hili. Pia wengine hulitumia kama eneo la mkutano ama dira la kumwongoza mtu iwapo amepotea jijini lakini sasa tunataka liwe pia mahali ambapo Wakenya wanazuru mara kwa mara ili kujifunza historia ya nchi, viongozi na matukio mbalimbali,” alisema Bw Okumu.

National Archives huwa inawachapishia vitabu watu ambao wangependa historia hio ihifadhiwe kwa njia hiyo.

Katika maonyesho, picha hizo kubwa ambazo zilizoashiria hatua tofauti katika maisha ya Mzee Moi kama vile ujana wake, familia, akiwa rais na kadhalika zilipangwa huku zikivutia mamia ya watu waliokuwa wakizitazama, kuzipiga picha na hata kuuliza maswali kuzihusu.

Picha iliyovutia watu wengi mno ni ile iliyokuwa na maneno ambayo alinukuliwa akisema Mzee Moi.

Miongoni mwa kauli zake zinazokumbukwa ni kama vile, “Siasa mbaya maisha mabaya”, “Uongozi ni zaidi ya urafiki”, “Tingisa kidole nione kama nyinyi ni watu wa KANU”, “Na nyinyi mkae kwa KANU.

Na Mungu awabariki. Mkae hivyo hivyo.”? Maneno mengine yaliyonukuliwa ni, “Nasikia watu wakisema ooh KANU itaanguka kura. Ooh KANU itashindwa. Nataka kuwaambia nyinyi kuwa KANU itatawala kwa miaka mia moja ijayo”.

Pia kulikuwa na maandiko, “Kama iko mtu ametukana mimi namsamehe. Na kama yuko mtu ambaye nimesema kitu imeumiza roho yake naomba msamaha” na “Pesa haiwezi kutatua shida zako zote. Lazima uombe Mungu pia atakusaidia kwa shida zako,” miongoni mwa mengine mengi.

Lakini kulingana na wasimamizi wa jumba hilo, si mambo kumhusu Mzee Moi pekee yaliyohifadhiwa humo bali kuna mengi mengineyo.