Makala

TAHARIRI: Tumuunge mkono Rais kuhusu ufisadi

January 28th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

MNAMO Januari 9, 1970, rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta aliwateua watu saba wakiongozwa na Duncan Ndegwa, kuchunguza masuala yaliyowahusu wafanyikazi wa umma, isipokuwa wanajeshi.

Tume hiyo iliwasilisha ripoti yake kwa Mzee Kenyatta Mei, 1971 na miongoni mwa mapendekezo yake lilikuwa lile la kwamba mfanyikazi wa serikali aamue kati ya kuitumikia serikali na kuwa na biashara za kibinafsi zinazoingiliana na majukumu yake.

Ilibainika wakati huo, na hata sasa, kwamba kuna wafanyikazi wa serikali wanaotekeleza majukumu yao na pia wanafanya biashara zinazokinzana na majukumu hayo.

Kwa mfano, afisa polisi wa trafiki anapaswa kuhakikisha watumiaji barabara wanatii sheria za barabarani.

Afisa huyo anapokuwa na biashara ya uchukuzi wa umma, hatakuwa na nguvu za kumkabili dereva anayemfanyia kazi, au kulikamata gari lake likiwa limekiuka sheria hizo.

Vivyo hivyo, kuna madaktari katika hospitali za uuma ambao wana hospitali, kliniki au maduka yao ya kuuzia dawa. Daktari kama huyo ataangalia kwanza faida inayoingia kwenye hospitali na kemisti yake badala ya kuhudumia wagonjwa.

Ni madaktari kama hawa ambao huwaandikia wagonjwa waende kununua dawa hata kama zinapatikana hospitalini.

Mwishowe, wananchi huishia kuilamu serikali kwa kufanya gharama ya matibabu kuwa juu mno kwa watu wa mapato ya kadri.

Ipo mifano mingi ya wafanyikazi wa umma ambao hutumia muda mwingi kushughulikia kazi na biashara zao, badala ya kuwapa wananchi huduma wanazostahili.

Ni sababu hii iliyomfanya Rais Uhuru Kenyatta kumwamuru Mwanasheria Mkuu, Paul Kihara kuandika mapendekezo ya kisheria kutekeleza ripoti ya Ndegwa.

Ufisadi Kenya unaendelezwa kwa sababu kila mtu ananufaika nao. Iwapo tutafanya iwe kosa ambalo mtu anashtakiwa na kuhukumiwa mara moja, hakutakuwa na haja ya kuwepo mabishano kama yanayoshuhudiwa sasa kati ya vitengo mbalimbali vya kushughulikia na utekelezaji wa haki.

Idara ya Mahakama imejitetea vya kutosha kuwa inashughulika tu na kesi kulingana na ushahidi unaowasilishwa. Ingawa huo ni ukweli, Jaji Mkuu David Maraga anapaswa kusoma kwa makini ripoti ya Bodi ya Sharad Rao, ili aelewe jinsi mahakimu na majaji wanavyotumiwa kuishinda haki.