Michezo

Tunaangazia mechi nane za Super 8 Jumapili

March 29th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MASHABIKI wanatarajiwa kushuhudia mechi nane ngumu za Ligi Kuu ya Super 8 Jumapili katika viwanja mbalimbali vya Nairobi.

Mabingwa watetezi Jericho All Stars watajibwaga uwanjani kujaribu kutetea rekodi yao watakapokabiliana na Githurai All Stars katika mechi itakayoanza saa kumi, ugani Camp Toyoyo.

Kabla ya mechi hiyo, Makadara Junior League SA wataikaribisha Kawangware United mapema uwanjani humo kuanzia saa saba.

Baada ya majuzi kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Team Umeme na kushuka hadi nafasi ya tatu, Jericho wanatarajiwa kucheza kwa makini kuepuka kipigo kingine.

Tayari mshambuliaji wao matata, Kelvin Ndungu amefunga mabao matatu katika mechi tatu, msimu huu.

“Kwa sasa mawazo yetu yanalenga mechi ya kesho, Tumekuwa na wakati mzuri wa kujiandaa kwa pambano hilo huku tukitarajia kupata matokeo,” Ndung’u alisema.

Githurai All Stars ambao mwaka uliopita ndio waliotwaa ubingwa wa Super 8 Daraja la Kwanza wataongozwa na mshambuliaji wao matata Joe.

Abongo alifunga mabao 27 msimu uliopita, lakini huenda mambo yakawa magumu kwake leo atakapoongoza wenzake dhidi ya Jericho ambao pia wana safu nzuri ya ushambuliaji ikiongozwa na nahodha Njuguna na Daniel Kago.

“Tumejiandaa kucheza mechi yetu bila wasiwasi wowote,” alisema kocha wa Githurai, Fredrick Ochieng.

Uwanjani Nakeel, vinara Metro Sports watakuwa ugenini kucheza na Rongai All Stars wanaoshikilia nafasi ya saba jedwalini, huku Meltah Kabiria wakivaana na Dagoretti Former Players FC ugani Riruta BP.

 

Ratiba ya mechi za Jumapili

Shauri Moyo Sportiff na MASA (Makongeni, saa tisa); Rongai All Stars na Metro Sports FC (Nakeel, saa tisa); Makadara Junior League SA na Kawangware United (Camp Toyoyo, saa saba); Jericho All Stars na Githurai All Stars (Camp Toyoyo, saa kumi); Meltah Kabiria na Dagoretti Former Players FC (Riruta BP, saa tisa); Huruma Kona VS Team Umeme (Huruma Kona, saa tano); TUK na NYSA (Kabete Cavs, saa tisa); Mathare Flames na Lebanon FC (Drive In grounds, saa tisa).