Habari Mseto

Tunaheshimu Seneti, Matiang'i atoa hakikisho

October 12th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama, Fred Matiang’i amekanusha madai kwamba mawaziri hudharau Seneti kwa kukaidi mialiko ya kufika katika bunge hilo.

Akiongea na wanahabari baada ya kuongoza mawaziri tisa katika mkutano na uongozi wa Seneti, Dkt Matiang’i hata hivyo aliungama kuwa baadhi ya mawaziri huchelewa kufika mbele ya kamati za Seneti.

“Lakini tukichelewa mimi na wenzangu huwasiliana na wenyeviti wa kamati husika mapema na kutoa sababu zetu. Madai kwamba tunaidharau seneti sio ya kweli kwa sababu hawa ni wawakilishi wa wananchi ambao sote tunahudumia,” akasema.

Dkt Matiang’i alikuwa ameandamana na mawaziri James Macharia (Uchukuzi), George Magoha (Elimu), Mutahi Kagwe (Afya), Sicily Kariuki (Maji), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Farida Karoney (Ardhi).

Kuhusu madai ya kucheleweshwa kwa majibu ya maswali kutoka kwa maseneta, Dkt Matiang’i alisema hali hiyo huchangiwa na haja ya kutoa majibu na maelezo ya kina.

“Huwa tunataka kutoa majibu na taarifa zenye maelezo yote yanayohitajika ili kufaidi wananchi wanaowakilishwa na maseneta hawa. Sio kutokana na dharua inavyodaiwa huko nje,” akaeleza Matiang’i ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Shirikishi ya Mawaziri kuhusu Utekelezaji wa Miradi na Mipango ya Serikali Kuu.

Wenyeviti wa kamati za seneti wamekuwa wakilalamika kuwa maseneti hukaidi mialiko ya kutakiwa kufika mbele ya kamati zao, hali inayoathiri utendakazi wa kamati hizo.

Baadhi ya mawaziri ambao wameelekezewa lawama hizo ni Dkt Matiang’i mwenyewe, Bw Macharia (Uchukuzi) Bi Karoney (Ardhi) na Kagwe (Afya).