Habari Mseto

Tunataka kuwapa wasomaji wetu picha za hali halisi, New York Times yajitetea

January 16th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

SHIRIKA la habari kutoka Marekani New York Times limesukumwa hadi ukutani na Wakenya na wasomaji wake kwa jumla, hadi likaomba msamaha, baada ya kuchapisha picha za wafu wa vamizi la hoteli ya Dusit, jijini Nairobi.

Kupitia ujumbe Jumatano, shirika hilo la habari lilisema “Tumepata habari kuwa baadhi ya wasomaji wetu wameghadhabishwa nasi kwa kuchapisha picha za wafu katika vamizi la Nairobi.”

“Tunaelewa uchungu wa habari hiyo na tunajaribu tuwezavyo kuhakikisha kuwa maneno na picha tunazotumia wakati kama huu zinafaa,” likasema.

Picha zilizochapishwa na shirika hilo zilionyesha mili ya watu katika hoteli hiyo, na manusura waliojaa damu.

Picha hizo zilizua pingamizi kali kutoka kwa wasomaji na watumiaji wa mitandao ya kijamii, wakilitaka kuziondoa mara moja na kusema kuwa lengo lao halikuwa zuri.

Hata hivyo, shirika hilo bado halijaondoa picha zenyewe kutoka mitandao yao.

“Tunataka kuwaheshimu walioathirika katika vamizi hilo. Lakini pia ni muhimu kuwafahamisha wasomaji wetu picha halisi ya vamizi la aina hii- hii inajumuisha kuonyesha picha ambazo zinatoa taswira ya hali ilivyo,” shirika hilo likasema kupitia habari Jumanne.

New York Times iliendelea kusema kuwa kote duniani inatumia mkondo huo wakati matukio ya aina hiyo yanapotokea, kwa kusawazisha hitaji la heshima kwa waathiriwa na kuonyesha ukweli wa yanayotendeka.