Habari MsetoSiasa

Tunatambua umuhimu wa Mau, watu wafurushwe – Chepkut

September 8th, 2019 1 min read

Na Titus Ominde

MBUNGE wa Ainabkoi Bw William Chepkut ameunga mkono kufurushwa kwa watu kutoka Msitu wa Mau lakini akaomba shughuli hiyo ifanywe kwa kuzingatia utu.

“Tunajua umuhimu wa msitu huu kwa Wakenya, kile ambacho naomba ni utu kuzingatiwa wakati huu wa kufurusha watu kutoka msitu huo,” alisema Bw Chepkut.

Akihutubu mjini Eldoret, Bw Chepkut aliitaka serikali iwafidie watu wenye vyeti halali vya umiliki ardhi katika msitu huo.

Anawataka wanasiasa wenzake waache siasa za ubinafsi katika shughuli hiyo, huku akitaka wamiliki wa vyeti halali wapewe ardhi mbadala.

“Kuna watu ambao wamekuwa wakiishi katika msitu huu baada ya kununua ardhi husika kutoka kwa serikali, watu kama hao wanapaswa kufidiwa na serikali,” alisema

Chepkut ambaye alionekana kutofutiana na viongozi wengine kutoka Rift Valley ambao wanapinga kufurushwa kwa watu kutoka katika msitu huo alisema utunzi wa msitu haupaswi kuingizwa siasa za ubinafsi.

“Suala la kulinda msitu wa Mau halipaswi kutumiwa kama kigezo cha siasa za 2022, zote kama viongozi tunapaswa kutafuta mbinu muafaka ya kuifadhi msitu huu,” alisema Bw Chepkut.