Habari Mseto

Tunateseka, wakazi Lamu waitakata serikali kuwarudisha madaktari wa Cuba

May 28th, 2019 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Lamu wanaililia serikali ya kitaifa kuwarudisha madaktari wa Cuba ambao waliondolewa kwenye kaunti hiyo mwezi mmoja ulioppita.

Mnamo Aprili 15 mwaka huu, serikali iliwaondoa madaktari wote wa Cuba waliokuwa wakihudumu kwenye kaunti nne zinazopakana na Somalia, ikiwemo Lamu, Garissa, Wajir na Tana River baada ya madaktari hao kuhofia usalama wao.

Wasiwasi wa madaktari hao wa Cuba ulichangiwa na kisa ambapo wenzao wawili waliokuwa wakihudumu kwenye kaunti ya Mandera walikuwa wametekwa nyara na magaidi wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab ambao waliwavukisha nchini Somalia.

Hadi sasa madaktari hao hawajaonekana.

Wakizungumza na Taifa Leo kisiwani Lamu Jumatatu, wakazi walieleza kutoridhishwa kwao na hatua ya serikali ya kuwaondoa madaktari hao.

Walisema tangu madaktari hao walipoondoshwa eneo hilo, hali ya matibabu kwenye hospitali za Lamu haijakuwa sawa.

Wakazi wanasema wamekuwa wakikosa huduma muhimu ambazo madaktari hao wa kigeni walikuwa wakitoa hospitalini, hatua ambao wanasema imeweazidishia dhiki wagonjwa.

Bw Ali Loo alisema kuondoka kwa madaktari hao kumepelekea sekta ya afya kaunti ya Lamu kurudi kama zamani ambapo kesi nyingi za wagonjwa sasa zimeanza kupewa rufaa hospitali za nje.

“Tungeiomba serikali kuu kutuonea imani sisi wakazi wa Lamu. Warudishe madaktari wetu wawili wa Cuba ili kuendelea kuhudumia hospitali zetu za Lamu. Tumeanza kushuhudia rufaa nyingi za nje ya Lamu kwani huduma ambazo madaktari hao walikuwa wakitoa hazipatikani tena,” akasema Bw Loo.

Bi Khadija Abdalla aliikashifu serikali kuu ya kuendelea kutelekeza kaunti ya Lamu kihuduma.

Alisema hajafurahishwa na uamuzi wa serikali wa kuondoa madaktari wa Cuba Lamu, ikizingatiwa kwamba eneo hilo kwa sasa ni salama licha ya kwamba linapakana na Somalia.

Aliisisitizia serikali kubadili msimamo wake na kuwarudisha madaktari wa Cuba eneo hilo.

“Lamu ni salama na sielewi kwa nini kisa kilichotokea Mandera kiathiri utendakazi wa madaktari wa Lamu. Kuondolewa kwa madaktari hao hapa kwetu ni dhihirisho tosha kwamba utelekezaji wa kaunti yetu kihuduma na maendeleo ambao umeshuhudiwa kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru wan chi hii umeanza kurudi tena. Lamu iko na amani na madaktari warudishwe,” akasema Bi Abdalla.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo aidha ulibaini kuwa idadi ya wagonjwa wanaozuru kwenye hospitali kuu ya King Fahad katika siku za hivi karibuni imepungua hasa tangu madaktari wa Cuba kuhama.

Utawala wa hospitali hiyo awali ulikuwa umetangaza kuwa idadi ya wagonjwa wanaozuru hospitalini ilipanda kwa kiasi kikubwa kufuatia ujio wa madaktari wa Cuba.

Kwa upande wake, Daktari Mkuu Msimamizi wa hospitali Kuu ya King Fahad mjini Lamu, Sagaf Mashra alisema matumaini ya madaktari hao wa Cuba kurudi Lamu ni finyu kwani tayari walizuru Lamu kwa mara nyingine na kuchukua kila kilicho chao na kwenda zao.

“Madaktari walirudi Lamu kuchukua vitu vyao vyote na kwenda zao. Hadi sasa hatujapata mawasiliano yoyote na sidhani madaktari hao watarudi tena kuhudumu eneo hili,” akasema Bw Mashrab.