Habari MsetoSiasa

Tunateswa na mabosi wetu, wafanyakazi wa wabunge walia

October 8th, 2018 1 min read

Na SAMWEL OWINO

WAFANYAKAZI wa wabunge wamelalamika kuhusu mateso wanayopitia mikononi mwa baadhi ya wabunge.

Mmoja wa wasaidizi wa kibinafsi wa mbunge mmoja kutoka Kaunti ya Kitui, alieleza jinsi alivyofutwa kazi mnamo 2014, siku mbili kabla afanye harusi.

Alieleza jinsi mnamo Desemba 4, 2014, alikuwa akinunua nguo za harusi mtaani Eastleigh, Nairobi, kisha hakusikia simu ikilia na baadaye alipoangalia alikuta mbunge amemtumia ujumbe mfupi kumwarifu amesimamishwa kazi.

“Niliangalia simu yangu saa mbili baadaye nikapata alijaribu kunipigia simu, na kulikuwa na ujumbe kwamba nimesimamishwa kazi. Niliendeleza maisha yangu lakini unaweza kufikiria nilivyohisi, kufutwa kazi siku mbili tu kabla kufanya harusi,” akasema.

Mwingine alieleza jinsi mke wa mbunge alivyomwambia avunje sheria za barabarani ili kuepuka msongamano wa magari jijini lakini polisi walipotokea, mke huyo wa mbunge aliita teksi na kumwacha akakamatwa.

Alifikishwa kortini siku iliyofuata na kutozwa faini ya Sh30,000 na ikabidi mamake amlipie.

Walinzi, madereva na wasaidizi wa kibinafsi wa wabunge tuliozungumza nao walieleza jinsi wanavyofanya kazi kwa masaa mengi na wakati mwingine hufanyishwa kazi zisizostahili.

Madereva hasa walisema wao huambiwa wapeleke watoto wa waajiri wao shuleni, mara wapeleke wake za wabunge saluni, huku wengine wakilazimika kutazama na kumeza mate wabunge wanapokuwa karamuni na katika sehemu za burudani.

Karani wa Bunge, Bw Michael Sialai, alisema matukio hayo yalikuwa mengi katika bunge lililopita lakini yalitatuliwa.

Alisema malalamishi mengi yalikuwa yakihusu kufanya kazi kwa muda mrefu kwa siku, na kucheleweshwa kwa mishahara ya wafanyakazi hao.

Aliambia wafanyakazi wanaotumikia wabunge wawe wakipiga ripoti rasmi kwa wabunge hao na wasimamizi wa maeneobunge.