Makala

‘Tunatiwa presha tuzae watoto wa kusaidia waume kulisha mifugo’

March 24th, 2024 3 min read

NA OSCAR KAKAI

WANAWAKE katika Kaunti ya Pokot Magharibi sasa wanadai kwamba waume wao kazi yao ni kulisha mifugo na kurejea nyumbani kutaka kuwapachika mimba tu, bila kutafakari kuhusu umuhimu wa upangaji uzazi.

Baadaye waume wao wanarejea malishoni kuchunga mifugo yao.

Walisema bado kuna baadhi ya wanaume ambao huzembea na kazi yao ni kulala chini ya miti wakingoja wake zao kuleta chakula nyumbani.

Wanawake waliteta baadhi ya wanaume hutaka akina mama kuzaa watoto wengi kwa sababu ya lengo la kupata watoto wanaoweza kuwasaidia kuchunga mifugo.

Akina mama ambao jukumu lao ni kulisha familia, sasa wako na uzito wa familia kubwa bila kusaidiwa na waume wao.

Kasumba na mila kuwa watoto wengi ni ishara ya mali nyingi, vimelemaza juhudi za kufakinisha mpango wa uzazi katika jamii za wafugaji.

Wanawake wengi eneo hilo wanaumia kutokana na kiangazi na baa la njaa sababu wanaume wao hawawasaidii.

Mnamo mwaka wa 2018, wanaume wengi katika kaunti ya Pokot Magharibi walipinga suala la wanawake kupanga uzazi.

Kumekuwa na visa vya wanaume kuangalia mapaja na juu ya mikono kuhusu mbinu za uzazi ikiwa zimetumika kwao suala ambalo huleta fujo kwa familia.

Jane Cheyech, 34 (sio jina lake halisi) mama wa watoto wanne katika kijiji cha Serewo anasema kuwa amekuwa akitumia mbinu za kisasa za kupanga uzazi kwa muda wa miaka sita lakini mumewe hajui.

“Huwa ninaomba asigundue. Sisi hupambana kulisha watoto sababu sisi wote hatuna kazi maalum ya kutegemea,” anasema Cheyech.

Si yeye pekee anayepanga uzazi kisiri kwa kuogopa mume kujua.

Kijijini kwao kuna wengi wanaofanya hivyo chini ya maji kwa sababu waume wanaamini kuwa watoto wengi ni kigezo cha mali.

Alice Cheptoo kutoka Chepareria anasema kuwa wanaume katika jamii za wafugaji mara nyingi hufurahia mama akipata mimba ambapo wanasherekea bila kujali maisha ya mtoto yatakuwaje.

“Wanaume hufanya maamuzi kwa jamii na kile wanawake wanafanya, huamuliwa na wanaume,”anasema Bi Cheptoo.

Susan Krop, mwenyekiti wa kikundi cha Kong’elai Women Network anasema kuwa wanawake wengi hawapangi uzazi sababu ya pingamizi kutoka kwa waume wao.

Anaongeza kusema kuwa familia za wanawake wengi eneo hilo zimeathirika na kiangazi sababu wanaume wengi huhamia nchi jirani ya Uganda kutafuta maji na nyasi.

“Wengi wameshindwa kupeleka watoto shuleni sababu hawana karo. Mambo yamebadilika kutokana na kiangazi. Tumeona akina mama wakifariki wakati wa kujifungua kila mwaka. Miili yao imedhoofika sababu hawana chakula,” asema Bi Krop.

Bi Emily Partany, mhudumu wa kupeana hamasisho kwa jamii, anasema kuwa wanaume wamekuwa kizingiti kwa kupanga uzazi.

Aidha alisema akina mama hulazimika kuenda kuchimba dhahabu kwenye migodi ili kulisha familia zao.

“Tunajaribu kubadilisha hali kwa kuwaambia wanaume kuwajibika pamoja na wake wao. Wakati mwingine, unakutana na mama kwenye migodi lakini wazee wao wanachunga mifugo,” asema Bi Partany.

Anasema kuwa wanawake hujenga nyumba zao sababu wazee huwa wako malishoni.

“Kutosoma kumechangia akina mama kuumia. Wakati mwingine, wanaume hupotea nyumbani mwaka mzima na mama hukarabati nyumba ikianguka,” asema.

Bi Partany anasema kuhusu suala la upangaji uzazi, hata wanaume hupiga sachi kwa miili ya wake zao ikiwa wametumia mbinu za kupanga uzazi.

Mratibu wa shirika la Declares Kenya, Jefferson Mudaki anawataka wakazi kupanga uzazi ili walee wana wao vyema bila matatizo kutokana na idadi nyingi ya watu nchini.

Anasema kuwa ni vyema kupanga uzazi na kupangia maisha ya watoto.

“Idadi ya watoto ni muhimu kwa kuwalea. Watu wawe na familia ambazo zinalingana na rasilimali ambazo wako nazo. Katika eneo hili mama mmoja huwa na watoto kati ya sita na saba,” akaeleza Bw Mudaki.

Aliwataka wanaume na wanawake kujumuishwa kwa kupanga uzazi.

Afisa wa lishe bora katika kaunti ya Pokot Magharibi Leah Chelopay anasema kuwa wanaume kwenye kaunti hiyo wameulaumiwa kwa kuwapa mzigo akina mama kutokana na ongezeko la utapiamlo kwenye kaunti hiyo.

“Lishe mbaya ambapo wanaume hawafanyi kazi na kuwaachia akina mama mzigo wa kutafuta chakula ni tatizo kuu,” asema Bi Chelopay.

Kaunti ya Pokot Magharibi ina uzao wa juu wa asilimia 6.7 hiyo ikiwa saw aba watoto kati ya sita na saba kwa kila mwanamke.

Kaunti hiyo ni ya pili kwa mimba za mapema kwa asilimia 36 kutoka kwa asilimia 29 mwaka wa 2014 huku kaunti ya Samburu ikiwa na asilima 50 kulingana na ripoti ya afya ya mwaka wa 2022 ya Shirika la Takwimu Nchini, yaani Kenya National Bureau of Statistics (KNBS).

[email protected]