Tunatoa huduma muhimu, tupewe chanjo ya corona, wasema wanabodaboda

Tunatoa huduma muhimu, tupewe chanjo ya corona, wasema wanabodaboda

Na LAWRENCE ONGARO

WAHUDUMU wa bodaboda mjini Thika wameitaka serikali kuwajumuisha kwa vikundi vitakavyopokea chanjo ya Covid-19.

Kiongozi wao Bw Maina Irungu alidai wanabodaboda wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa corona kutokana na huduma wanayotekeleza kwa umma.

Alieleza kuwa miongoni mwa vikundi vilivyopendekezwa kupokea chanjo hiyo kama wahudumu wa Afya, walinda usalama na walimu, wao pia wangetamani kujumuishwa kwani wanatoa huduma muhimu za kila siku.

Aidha, alieleza kuwa kazi yao ni muhimu kwa sababu wanawabeba watu wa tabaka mbalimbali.

Bw Stephen Kiragu ambaye pia ni mhudumu wa BodaBoda alidai wananchi popote walipo wanastahili kufuata maagizo ya afya ili kuzuia corona.

“Siku hizo watu wengi hawazingatii kuvalia barakoa na kunawa mikono. Ni vyema wakufuata maagizo ya wizara ya afya, ” alisema Bw Kiragu.

Aleleza ya kwamba wananchi wameonyesha kulegeza kamba dhidi ya kupambana na covid-19.

Kulingana na ripoti ya serikali dosi milioni moja za chanjo hiyo zilifika nchini Jumanne usiku kabla ya kusambazwa katika maeneo yaliyopendekezwa.

Lakini kulingana na Waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe, bado itachukua muda fulani kabla ya chanjo ya kutosha wakenya wote kuwasili hapa nchini.

Wataalam wa kiafya wamesema ya kwamba virusi vya covid-19 vinaendelea kuenea huku wananchi wakishauriwa kufuata maagizo ya afya ya kuvalia barakoa, kunawa mikono na kuweka nafasi ya mita moja unusu kutoka kwa mwenzako.

You can share this post!

Maeneo hatari kwa usalama Mathare yaorodheshwa

Austria, Denmark zavunja uhusiano kuhusu chanjo ya corona