Habari za Kitaifa

Tunazima kabisa uhasama wa kikabila Sondu – Kindiki

May 9th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI, kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani, imepiga marufuku ubebaji wa silaha kiholela katika eneo la Sondu kwenye mpaka wa kaunti za Kericho na Kisumu huku kambi ya kudumu ya maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia (GSU) ikibuniwa hapo kukomesha mapigano ya kila mara.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki mnamo Jumatano aliwaambia maseneta kwamba kambi hiyo itapewa uwezo zaidi kwa kuongezewa idadi ya maafisa na vifaa hitajika.

“Kando na hayo, wizara yangu imetoa amri kwamba maafisa wa polisi wanaohudumu katika kaunti zote mbili watakuwa wakishika doria eneo hilo usiku na mchana kuzuia uwezekana na kutokea mashambulio,” Prof Kindiki akasema.

Waziri aliongeza kuwa washukiwa kadhaa ambao walimakatwa kuhusiana na mapigano ya kikabila yaliyotokea eneo hilo mwaka 2023 walishtakiwa.

“Ningependa kulihakikishia bunge hili la Seneti kwamba wizara yangu inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa amani imedumu katika eneo hilo la Sondu. Katu masuala ya mipaka hayafai kusababisha vita kwani kuna njia za kuyashughulikia kwa amani,” akasema.

Waziri alisema hayo alipokuwa akijibu swali kutoka kwa Seneta wa Kisumu Tom Ojienda aliyetaka kujua kile ambacho serikali inafanya kuwapokonya silaha wapiganaji ambao hutekeleza mauaji Sondu kila wakati.

Mnamo Oktoba 2023, watu saba waliuawa eneo hilo na mali ya thamani kubwa ikaharibika kufuatia uvamizi uliotekelezwa na wahuni waliodaiwa kutoka upande wa Kericho.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki. PICHA | MAKTABA

Mnamo Jumatano, waziri aliwaambia maseneta kwamba serikali itawatumia wazee kutoka kaunti zote mbili na wanasiasa, kuendesha kampeni ya kuhubiri amani na utangamano katika eneo hilo.

“Nina furaha kwa sababu juzi magavana wa kaunti hizi mbili walikutana kujadili mipango ya kukomesha uhasama kati ya jamii mbili zinazoishi eneo hilo. Aidha, Prof Anyang’ Nyong’o wa Kisumu na Eric Mutai wa Kericho waliahidi kuingilia kati ili kukomesha maovu kama wizi wa mifugo. Wizara yangu inaunga mkono juhudi kama hizo,” waziri Kindiki akaeleza.

Prof Kindiki alisema asasi za serikali kama vile Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) pia zinaendesha shughuli za kuleta amani na utulivu eneo hilo.

Kando na mzozo wa mpaka kati ya Kisumu na Kericho, waziri huyo alisema kuwa kuna kaunti nyingine 25 nchini ambazo zinakumbwa na mizozo kama hiyo.

“Tutajaribu kadri ya uwezo wetu na kwa ushirikiano na ninyi kama viongozi, kupata suluhu ya kudumu kuhusiana na mizozo hiyo,” Prof Kindiki, ambaye ni Seneta wa zamani wa Tharaka Nithi, akawahakikishia maseneta.