Makala

Tunda lisilo na mvuto ingawa linaaminika kutibu kisukari, hata saratani

April 13th, 2024 1 min read

NA PETER CHANGTOEK

BAADHI ya watu hawapendi kula matunda ya kiwano kwa sababu ya ladha yake. Linapokuwa bichi, tunda hilo huwa na ladha ya mchanganyiko wa ndizi, ndimu, tango na tikitimaji. Lililoiva lina ladha kama ya tango.

Tunda la kiwano, linalojulikana sana kama thorn melon, aidha, lina protini, vitamini, na madini ambayo ni muhimu katika mwili, linapoliwa.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika jarida la International Journal of Biological Innovation, tunda hilo lina maji asilimia 80, ambayo husaidia kuondoa chembechembe zinazoweza kudhuru mwili.

Jarida hilo linaeleza kuwa, tunda hilo huwa haliwasaidii tu watu walio na ugonjwa wa saratani, bali pia husaidia kutibu ugonjwa wa kisukari unapogunduliwa mapema.

Tunda la kiwano lililokatwa vipande vinne. PICHA|PETER CHANGTOEK

Kiwano pia, husaidia kuimarisha afya ya ubongo pamoja na moyo. Isitoshe, huimarisha viungo vya damu na neva.

Aidha, tunda hilo la kiwano lina Vitamini A, ambayo husaidia macho kuona vizuri. Pia, kiwano husaidia kudhibiti homoni za msongo wa mawazo.

Tunda hilo pia lina Vitamini C. Aidha, lina Vitamini D na kalisiamu, ambayo husaidia kuimarisha mifupa na kusaidia kutibu magonjwa ambayo huathiri mifupa.

Vitamini  E  iliyoko kwenye kiwano husaidia kakabili chembechembe kwenye mwili, zinazoweza kusababisha magonjwa sugu; kama vile ugonjwa wa moyo na saratani.

Mkulima aonyesha matunda ya kiwano aliyoyachuma katika Kaunti ya Makueni. Matunda hayo yana manufaa kiafya. PICHA|PETER CHANGTOEK

Mbegu za kiwano zina aina fulani za asidi mafuta, kama vile linoleic acid na oleic acid. Asidi aina ya oleic, ambayo pia hupatikana katika mafuta ya zeituni, husaidia kupunguza shinikizo la damu.

Tunda la kiwano pia, lina madini ya chuma na zinki, ambazo hufanya vidonda kupona haraka na kutengeneza seli za damu na kudhibiti kiwango cha haemoglobini kwa damu.

Kiwano huwa na madini ya magnesi, ambayo hudhibiti kiwango cha sukari katika damu, na kuimarisha ufyonzaji wa vyakula kwa mwili.

Pia, kiwano hutuliza matatizo ya tumbo na huwa na nyuzinyuzi zinazosaidia kwa mmeng’enyo (digestation) wa chakula. Husaidia pia kutovimbiwa tumbo. Pia, kiwano husaidia kutibu vidonda vya koloni.