Michezo

Tundo moto balaa KCB Edoret Rally

November 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

DEREVA Carl ‘Flash’ Tundo amenyakua taji la Mbio za Magari za KCB Eldoret Rally na kuhakikisha vita vya ubingwa wa mwaka 2019 vinasalia vya farasi wawili kati yake na Baldev Chager.

Akishirikiana na mwelekezi wake Tim Jessop katika gari la aina ya Mitsubishi Evolution 10, Tundo alikamilisha mbio hizo zilizojumuisha kilomita 108.5 (mkondo wa sita ulifutiliwa mbali) katika nafasi ya kwanza kwa saa 1:13:18.0.

Chager alianza duru hii ya saba vyema kwa kushinda mkondo wa kwanza wa kilomita 18.4 katika eneo la Kaptagat kwa dakika 12:06 dhidi ya Tundo (12:09).

Chager, ambaye pia aliendesha gari lake la Mitsubishi Evolution 10, alisalia mbele baada ya mkondo wa pili katika eneo la Bugar la kilomita 16.5 kabla ya kupoteza uongozi huo katika mkondo wa tatu katika eneo la Salabin.

Tundo alishinda mkondo wa nne ambao ulishuhudia Chager akirushwa hadi nafasi ya tatu nyuma ya Onkar Rai. Ingawa Onkar alitamba katika mkondo wa tano, Tundo alikuwa ameandikisha muda mzuri kuibuka bingwa wa duru ya Eldoret.

Mkondo wa sita ulifutiliwa mbalia kwa sababu barabara ya mashindano ilikuwa na matope mengi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo. Akipeleka gari la Volkswagen Polo, Onkar alifunga mduara wa tatu-bora kwa saa 1:24:09.