Tunisia waandamana kuhusu bei za vyakula

Tunisia waandamana kuhusu bei za vyakula

NA MASHIRIKA

TUNIS, TUNISIA

MAELFU ya raia nchini Tunisia, walifanya maandamano makubwa kulalamikia bei za juu za vyakula na mikakati ya kisiasa inayoendeshwa na Rais Kais Saied.

Mshirikishi kutoka vuguvugu la Citizens Against the Coup Coalition, ambalo ni mojawapo ya makundi yanayoongoza maandamano hayo, alisema kuwa wamekataa katiba mpya iliyopitishwa na kiongozi huyo bila kuwashirikisha raia.

Kulingana na Ali al-Arid, ambaye ni miongoni mwa maafisa wakuu katika kundi la Ennahda Movement, maandamano hayo yataendelea hadi pale serikali itarekebisha hali.

Waandamanaji hao waliandamana katika eneo la kati la jiji kuu, Tunis.

Watu hao pia walibeba bendera za nchi hiyo na mikate, wakitoa malalamishi kuhusu bei za juu za vyakula.Mwaka uliopita, Rais Saied alifanya mageuzi ya kisiasa, kwa kuvunjilia mbali taasisi kadhaa za kusimamia uchaguzi baada ya kulivunja bunge.

Mapema mwezi huu Mei, alitangaza mpango wa kisiasa nchini humo.

HALI YA AWALI

Waandamanaji wanamtaka rais huyo kurejesha nchi hiyo katika hali ilivyokuwa hapo awali, wakipinga hatua yake kuifutilia mbali tume huru ya uchaguzi.

“Raia wa Tunisia wanataka uwepo wa demokrasia. Saided amevuruga uchumi wa taifa hili kiasi cha kuwafanya mamilioni ya watu kukosa chakula,” akasema mwandamanaji mmoja.

Maandamano ya Jumapili ndiyo makubwa zaidi dhidi ya kiongozi huyo kushuhudiwa nchini humo katika miezi ya hivi karibuni.

“Ni wazi raia wengi wanataka nchi hii kurejea katika hali ya demokrasia,” akasema Samira Chaouachi, ambaye ndiye naibu kiongozi wa bunge lililovunjwa.

Kama njia ya kuwajibu watu wanaoandamana dhidi ya Saied, wafuasi wake walifanya maandamano sambamba kumuunga mkono.

Tangu alipochukua uongozi mwaka 2021, kiongozi huyo amekuwa akijiongezea mamlaka kwa kuvunja bunge na kuanza kutawala bila kuzingatia katiba.Alisema kuwa ataibadilisha katiba ya sasa kwenye kura ya maamuzi.

Wakati huo huo, hali ya kiuchumi ya Tunisia imetajwa kuwa katika hali mbaya.Imebainika kuwa serikali ya taifa hilo inaendesha mazungumzo na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ili kupata msaada wa kukwamua uchumi wake na matatizo yanayowakumba raia wake.

Wadadisi wanasema kuwa mikakati ya Saied imelitumbukiza taifa hilo kwenye mgogoro mbaya zaidi wa kisiasa na kiuchumi tangu maasi ya mwaka 2011, yaliyosambaa katika mataifa mengine ya Kiarabu kama Misri na Libya.

Kando na kulivunja bunge, alilivunja Baraza la Idara ya Mahakama, ambalo lilikuwa muhimu katika kutetea uhuru wa majaji na maafisa wengine wa idara hiyo.

“Tutaendelea na harakati zetu hadi pale tutarejesha nchi hii katika hali ya demokrasia na uhuru wa kujieleza,” akasema Tijani Tizaoui, aliye miongoni mwa waandamanaji.

Katiba ambayo taifa hilo lilipata mwaka 2014 ilitokana mazungumzo miongoni mwa wadau na makundi kadhaa ya kisiasa.

Hata hivyo, Saied amekataa miito ya kuyashirikisha makundi ya kisiasa kwenye mazungumzo kusuluhisha mzozo uliopo.

  • Tags

You can share this post!

Jumwa akataa kukatwa miguu UDA

Nafasi ya Joho Azimio kupepeta siasa Pwani

T L