Makala

TUONGEE KIUME: Kaka, kupigana au kuua kwa sababu ya mapenzi ni ujinga


INASEMWA kuwa wanaume hupigana kwa sababu ya mambo matatu;pesa, ardhi na wanawake. Ondoa pesa na mashamba hapa. Wanaume wamekuwa wakiripotiwa kila mara wakiuana kwa sababu ya wanawake.

Hivi visa vimechosha na kusema kweli ni vya kipuzi, havifai. Mwanamume kamili hafai kupigana, kuua au kujiua kwa sababu ya mwanamke asiye mwaminifu kwake.

Naam, nasema asiyemwaminifu kwa kuwa hasira za wanaotekeleza mauaji zinasababishwa wanawake kucheza kwingi. Inaweza kuwa kumcheza shere mpenzi wake au kuwa na mpango wa kando kwa walio katika ndoa.

Tuanze na huyu wa kucheza shere wanaume. Huyo hafai kufanya mwanamume kupigana kiasi za kuua.

Kwa hakika, ukijua anakucheza shere unafaa kushukuru na kujiondolea balaa kwa sababu anaweza kukutia kwenye shida. Ukigundua demu anagawa asali kwa jamii ya wanaume, enda upimwe ujue hali yako na uwe tayari kwa matokeo ya kila aina.

Ukipata uko shwari, msahau hata kama umewekeza dhahabu kwake. Ukipata umeathirika, shukuru Mungu uko hai na utafute jinsi ya kuendelea kuishi kama wengine walio katika hali sawa ambao wametoa bidii na kufaulu kuliko wasioathirika.

Hakuna haja ya kuua ujipate jela au ujiue uache raha ya dunia hii iliyo na vipusa watamu kuliko aliyekusababishia machungu.

Kwa huyu mke mchepukaji, kaka, badala ya hasira, na ninajua inauma, shukuru kujua tabia yake ukiwa bado hai kisha ufunge ukurasa na ufungue mwingine.

Kuna wanawake watamu na waaminifu katika ulimwengu huu. Na kumbuka, mwanamke asiye mwaminifu hawezi ni sumu inayokiuka polepole. Kupigana kwa sababu ya mwanamke mchepukaji ni ujinga wa hali  ya juu.

Hana thamani kwako, kando na nderemo zake chumbani, ambazo zinakusukuma upigane ukizikumbuka na ambazo anachuuza mtaani kama samosa.

Mwanamke asiyekupatia utulivu wa akili hawezi kuwa na tabia kama hii na makosa makubwa anayoweza kikufanyia sio kukufanya upigane na wanaume wengine, ni kukusamehe ukinusurika ukimpigania.

Anapoamua kugawa tunda kwa jamii ya wanaume huwa anakuwazia mazuri kweli? Kwa hakika, mwanamke anayefanya hivyo huwa anakuua ukiwa hai na unachoweza kufanya ukigundua tabia yake ni kumuacha aendelee na tabia yake badala ya kulipuka kwa hasira na kuchukua sheria mikononi mwako hatua ambayo ni kilele cha ujinga.

Kaka, jipende kwanza, jithamini badala ya kujawa na ujinga upigane kwa sababu ya mwanamke asiyekuthamini kwa kugawa tunda unaloamini ni lako.