Makala

TUONGEE KIUME: Kaka, kusuka mistari kwa demu ni sanaa inayohitaji ujasiri


VIPUSA wanalalamika kuwa mabarobaro wanawaharibia muda wakifuata njia ndefu kabla ya kuwapasulia mbarika kwamba wanawatamani.

Ni tatizo la akina kaka kufungulia akina dada moyo na kuwaambia wana wamezea mate.

Ni kupungukiwa na mistari na kutojiamini na hata ikiwa kipusa ana hisia kwako, anaweza kukushiba. Hii tabia ina hata wanaume walio katika ndoa. Mwanamume mzima anakosa ujasiri wa kuitisha mkewe haki yake ya ndoa.

Tabia hii, inawasinya akina dada na wanaweza kukuchukia.

Kuwa jasiri kunaweza kufanya mwanadada kukuchangamkia hata kama hauna kakitu. Hii ni kwa wale akina kaka wanaoamini kuwa wanawake wanaweza kumiminika kwao kwa sababu wana pesa.

Kuwa na uhakika na unachotaka kwa mwanadada kabla ya kuanza kumrushia mistari. Usianze kwa kujionyesha ulivyo mtu wa maana.

Usiwe mtu wa kutapatapa kama maji ya ugali kwenye sufuria. Usiwe mtu wa kuharibia vipusa wakati ukigugumiza, lakini ni lazima ujue kwamba mkono mtupu haulambwi.

Ni lazima ujipange kumpasulia mbarika katika mazingira yatakayomfanya asisimke, sio katika kibandaski, jitume kaka na hautavunjika moyo.

Kurusha mistari kaka ni sanaa ambayo mbali na ujasiri, kunahitaji ubunifu. Unapofanya hivi, usiahidi mwanadada kwamba utamuoa ukijua hauwezi.

Kama unataka dozi ya uroda, mwambie tu, akina dada wanaelewa, usisahau wao ni binadamu kama wewe. Kama unataka mshirika wa kusukuma maisha, mwambie vivyo hivyo.

Usitumie uongo, haudumu. Uongo utakufanya uharibie binti ya watu wakati ambao angetumia kujishindia mwenzi wake wa maisha.

Kama haufahamu kaka, akina dada hasa wanaowania ndoa hawataki mchezo na maisha yao.

Hivyo, ukimwingiza boksi kwa ahadi ya kumuoa, isiwe lengo lako ni kuchovya asali na kutembea wafanyavyo (au wapendavyo kufanya) wanaume wengi.

Hii ndiyo sababu mabinti wametupachika jina la wana wa mama mmoja kumaanisha wanaume wote wanapenda kuonjaonja wanawake bila kuwa na mustakabali mahususi kuhusu maisha yao.

Narudia, usiahidi mwanadada ndoa iwapo hauko tayari kufanya hivyo.

Mabinti huwa wanachoka na mwanamume anayejifanya bumbu wanapomkumbusha kuhusu ahadi yao ya kuwaoa.

Kaka, funguka iwapo umebadilisha nia lakini ujue inaweza kuwa hatari kwako. Jipange, jipe moyo na ufanye chaguo lako kwa uangalifu hivi kwamba unaporusha chambo, itakuwa vigumu kwa demu kukosa kukimeza.

Epuka kosa hili; kuchukulia mademu kama wajinga au vyombo vyepesi vya kudanganya. Hawa ni viumbe waliojaliwa busara na uvumilivu wa ajabu ambao wanaume wamekuwa wakitumia vibaya.

Iwapo wewe ni mmoja wa wanaochukulia wanawake kuwa wajinga, fikiria mara mbili na uache kuwaharibia muda ukiwaahidi ardhi na mbingu ikiwa nia yako sio kuwaoa.