Makala

TUONGEE KIUME: Mapenzi si miereka ya chumbani tu, tenga muda wa mtu wako

Na BENSON MATHEKA June 27th, 2024 2 min read

KAKA usiigize mahaba kwa kutaka ngono kila wakati, kuwa halisi; mapenzi ya dhati ni zaidi ya ngono. Mtu wako anataka kuwa karibu nawe.

Ngono ni rahisi kupata, lakini kufanya mapenzi kunahusisha moyo.

Kutenga muda wa kuwa na mtu wako ndiyo zawadi ya thamani zaidi unayoweza kumpa. Sio kujenga misuli na kudhani utaitumia kumkoleza mahaba chumbani usiku mmoja kisha unatorokea vilabuni. Unajidaganya. Kadiri ninyi wawili mnavyotumia muda pamoja kuzungumza, ndivyo urafiki unavyoongezeka. Urafiki unahitaji kubadilishana maoni na maneno ya kipekee. Kupenda ni kupatikana na kuzungumza. Kwa kufanya hivi mnajenga mvuto wa kihisia kwa kuwa kila mmoja anafichulia mwenzake mawazo yake.

 Hisia  za kweli huonekana wakati kama huo.

Hapa unakuwa na muda wa kumgusa mtu wako na kuelewa mwili wake vyema ili uweze kumshughulikia vyema.  Wakati nyinyi wawili mnabembelezana, kudekezana na kupapasana na kushikana mikono mnapanda mizizi ya mahaba.

Na usimwache mtu wako atafute chakula cha kiroho peke yake au kivyake. Tenga muda wa kuandamana naye kanisani na kujivinjari baadaye.

 Raha iliyoje kuliko kutoka kanisa na kumuacha mkeo kufululiza nyumbani ukielekea baa kutangamana na marafiki. Kaka, marafiki hawafai kutumia muda unaofaa kuwa na mkeo isipokujwa kwa jambo la kuongeza thamani maisha yako na bila shaka jambo hilo sio mvinyo.

Ninyi wawili mnapomfuata Mungu kama wanandoa, mnashirikiana pamoja, kuomba pamoja, kusoma neno la Mungu pamoja, kukemea na kukanyanga mapepo pamoja mnaibuka washindi. Ukiwa na muda wa kutosha kuwa na mkeo, atakuheshimu.

Na usiogope kuketi uchi ukiwa naye au kutochangamka akiwa hivyo mkiwa peke yenu nyumbani. Anafaa kujua mwili wako ndani na nje nawe unafaa kujua wake. Kumbuka, mke mume mzuri ni anayejua nguvu na

mapungufu ya mkewe.

Kwa kweli, wanawake wanajua  mapungufu ya waume zao kuliko waume wanavyojua ya wake zao. Unaweza kushangaa na huu ndio ukweli wa mambo. Hii ni kwa sababu wanaume hawana muda wa kutosha kuwa na wake zao isipokuwa wakati wa kuzima hanjam zao.

Usisubiri wakati wa magumu ndio ukaribiane na mtu wako. Ukitenga muda wa kutosha wa kuwa na mke wako utaepuka majaribu na kumwepushia yanayoweza kumjia pia. Kila wakati hisi ulimwengu ni wako na mtu wako pekee.

Hivi ndivyo unaweza kujenga mahaba ya hadi uzeeni. Ukikosa kutenga muda wa kuwa na mtu wako ukiwa na nguvu, utamtafuta umkose ukiwa mzee. Wanaokufanya umpuuze ukiwa na nguvu hawatakuwa utakapomhitaji kuwa karibu nawe. Kwa hivyo, kaka usifanye mtu wako chombo vya ngono. Anakuhitaji, mpe muda wake.