Makala

TUONGEE KIUME: ‘Maplayer’ ni watamu lakini watakuacha kwa mataa


VIPUSA huwa wanapenda kupuuza ushauri wakisema wanajua wanachofanya hasa wakionywa wasichumbie wanaume wasiomakinikia mapenzi.

Wale wanaume wanaofahamika kama ‘maplayer’ ambao kazi yao ni kuchangamkia vipusa, kuwaonja na kuondoka wakiwaacha wakisononeka. Anakupamba kwa sifa na maneno hadi unasahau kuna watu wengine duniani wanaokuwazia mazuri kisha baada ya mambo kukuendea yombo unakumbuka onyo ulilopuuza.

Unaweza kusikia kipusa akitetea uhusiano wake na mtu anayeonywa na wanaomjua vyema au walio na tajiriba ya mapenzi kwa kusema ‘najua ninachofanya, ameahidi kunioa’  kisha baada ya muda anaanza kulia akiachwa kwenye mataa baada ya kutumiwa akatumika.

Mademu kama hao huwa wako tayari kwa ndoa lakini wanaangukia mabarobaro wasio tayari na kuwaacha na maumivu makali ya moyo yanayoweza kuathiri maisha yao yote. Haya yanafanyikia vipusa kila siku.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema ni muhimu mwanadada kuwa na hakika kwamba mwanamume anataka kumuoa na anayeingia katika uhusiano wa mapenzi wa muda mrefu naye yuko tayari mwa ndoa.

“Unaweza kuwa tayari kwa ndoa lakini ukiolewa na mtu ambaye hayuko  tayari utakuwa umejitumbukiza katika kinu. Kuwa na hakika, usiungane na mtu mbaya ukiwa na nia nzuri ya kuwa na maisha yenye furaha,” aeleza Ivy Wachuka, ambaye ni mwanasaikolojia na mshauri wa ndoa.

Vipusa wanaopuuza onyo, mara nyingi huwa wanageuka kitoweo cha wanaume maplayer ambao wana uzoefu wa kuchota warembo kwa lengo la kuwatumia tu.

“Mara nyingi vidosho huwa wanapumbazwa na maisha ya hali ya juu ya maplayer na kufumba macho na masikio yao. Wanaamini kila wanachoona na kuambiwa na wanaume hao ambao wanawathamini tu wanapowatumia na kuwatoa katika mawazo yao wakiachana,” asema Wachuka.

Mwanasaikolojia huyo anasema kwamba hakuna makosa ya kufurahia maisha ya mapenzi lakini vipusa wanapaswa kufanya hivyo kwa kiasi, wakiweka mipaka na wanaume wanaotangamana nao kimahaba.

“Weka mipaka na mtu wako na wanaume kwa jumula, usipuuze onyo lolote kumhusu mwanamume lakini fanya uamuzi wako binafsi, lizingatie onyo, lichunguze,  usikubali mwanamume atawale mawazo yako kwa sababu kwa kufanya hivi hautaona upande mwingine wa maisha yake tofauti anavyojisawiri kwako,” aeleza Wachuka.

Kuruhusu chali atawale maisha yako na kukuamulia mambo ni kumpa madaraka yako yote na kuna majuto.

“Fahamu kwamba anavyojisawiri kwako au unavyomsawiri sivyo wengine wanavyomsawiri. Anaweza kujivika ngozi ya kondoo akiwa nawe  ilhali watu wengine wanamfahamu kama  mbwa mwitu,” asema Wachuka.