Makala

Tuongee Kiume: Usiwe mchoyo wa maneno matamu kwa demu wako

Na BENSON MATHEKA September 5th, 2024 2 min read

INASEMEKANA kuwa ulimi ni kiungo kidogo kinachoweza  kujenga au kuharibu kwa kutegemea unavyokitumia.

Kiungo hiki ni muhimu kwa kujenga au kubomoa uhusiano wowote wa kimapenzi.

Chunga unachopenda kuzungumzia, unavyokieleza  na wakati wa kukieleza.

Iwapo kila neno linalotoka kwa mdomo wako linakulenga wewe binafsi na sio wewe na mchumba wako, basi unatema sumu inayoweza kuua uhusiano wako. Ni kweli unapaswa kujipenda kwanza ili uweze kupenda mtu mwingine, lakini katika masuala ya uhusiano wa kimapenzi, unapaswa kusawazisha.

Isiwe unajifikiria tu. Isiwe kila wakati ni unachotaka au anachotaka kufanyiwa  na mtu wako. Hii inampa taswira ya wazi kuwa haumjali na ataanza kuhisi kwamba unamtumia na kwamba uhusiano ni wa upande mmoja ilhali unapaswa kuwa wa watu wawili.

“Muhimu kabisa,” aeleza Cindy Nyawira, mwanasaikolojia na mtaalam wa mahusiano, ni jinsi unavyoachilia kila neno kutoka kwa kinywa chako.

“Unaweza kuwa na jambo zuri au useme jambo kwa nia nzuri lakini uliseme kwa njia isiyotoa taswira na maana halisi ya ulichotaka kusema. Hii ndiyo sumu inayozua mafarakano katika ndoa,” aeleza Cindy.

Hapa ndipo unapata mtu ambaye hakubali makosa yake au anataka kila kitu kifanyike anavyotaka. Mtu ambaye hawezi kuomba mchumba wake msamaha lakini anatarajia asamehewe akikosa. Mtu ambaye hapendi kusikia maoni ya mchumba wake.

“Mtu wa aina hii huwa anafanya mwenzake kuhisi kwamba yupo katika uhusiano kuonekana tu na sio kuchangia kuujenga. Uhusiano ukiwa wa kutegemea maoni ya upande mmoja huwa sio uhusiano tena. Hali hii inaweza kuepukwa iwapo watu wanaweza kutumia vyema ulimi wao,” aeleza Cindy.

Ulimi ukikosa kutumiwa vyema matokeo huwa ni kuropokwa maneno yanayozua ugomvi na vita.

“Ugomvi hutokana na maneno yanayoudhi na mara nyingi huwa unazaa vita ambavyo mtu anaweza kuepuka,” aeleza Cindy.

Lakini usiwe mtu wa kupimia mwenzi wako maneno. Usiwe mchoyo wa maneno kwa mpenzi wako. Kuwa mchangamfu kwake, ukimchangamsha, anakuchangamkia. Uhusiano wa kimapenzi unajengwa kwa maneno matamu,” asema Tony Kimeu, mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya ndoa.

Anasema jinsi mtu anavyozungumzia mtu wake, ndivyo anavyojenga au kubomoa uhusiano wake. “ Maneno ya kupongeza, kutia shime na kudekezana yanajenga uhusiano lakini ya kutetesha, matusi, kudhalilisha na kukaripiana yanaubomoa,” aeleza Kimeu.