Pambo

Tupa jongoo na mti wake: Si vyema kuoa au kuolewa na Ex wako

May 12th, 2024 2 min read

NA BENSON MATHEKA

NDOA ni hatua muhimu katika maisha ya mtu, na ni muhimu kufanya maamuzi ya busara unapofikia hapo.

Ni muhimu unapoamua kuoa au kuolewa ujiepushe na waliokuwa wapenzi wako. Mtu huyo anafaa kuwa historia katika maisha yako. Tafuta mwingine kwa kuwa ndoa huwa ni kipindi kipya katika maisha.

“Kamwe usiwazie kuingia katika ndoa na mpenzi wako wa zamani, kuna sababu yeye ni mpenzi wako wa zamani. Ex wako anafaa kuwa sehemu ya historia yako na kuolewa naye ni sawa na kurudisha nyuma maisha yako,” aeleza mshauri wa mahusiano ya mapenzi, Jackline Watani.

Kwa vipusa na mabarobaro wanaopuuza ushauri wa wazazi kuhusu ndoa wakisema ni kuingiliwa kwa maisha yao au wanajua wanachofanya, Watani anawashauri kuwa kufanya hivyo ni kupanda mbegu ya majuto.

“Usiolewe na mtu ambaye karibu asilimia 70 ya wanafamilia wao hawakupendi. Uwezekano wa ndoa ya aina hii kutodumu ni mkubwa sana na pengine hautafurahia uhusiano huo,” anasema.

Hii, aeleza, ni kwa kuwa hawatakupatia nafasi ya kufurahia uhusiano wako na mume au mkeo.

Kabla ya kukata kauli kuolewa, mwanasaikolojia huyu anashauri watu kutofautisha uhusiano wa mapenzi au wa kurushana roho akisema haya ni mambo mawili tofauti na yanakanganya watu.

“Kuna watu wanaokuwa na uhusiano kwa ajili ya kurushana roho pekee na kuna wanaojenga uhusiano unaoelekea ndoa ambao huwa umekitwa kwa hisia za dhati za mapenzi. Ni muhimu kuelewa dhamira ya kuingia katika uhusiano,” aeleza.

Watani anasema ni makosa mtu kuingia katika uhusiano ili kujiondolea upweke.

“Ukiingia katika uhusiano kwa sababu ya upweke, matokeo yanaweza kuwa ya kutisha. Unafaa kuingia katika uhusiano wa mapenzi baada ya kuwa na uhakika una hisia za mapenzi kwa mtu. Unaweza kujiongezea mateso ukidhani mtu unayechangamkia atakusaidia kujiondoa katika upweke,” asema.

Na anaonya watu dhidi ya kufichua uwezo wao kamili wa kifedha au siri zao kwa mtu ambaye hawafahamu vyema.

“Ukiona mtu anachunguza uwezo wako wa kifedha siku za mwanzo za uhusiano wenu, hepa mapema. Huyo analenga ulicho nacho, hakupendi,” aeleza.

“Kabla ya kukata kauli kuanza maisha na mtu, unapaswa kutilia maanani maendeleo na ustawi wako kwanza. Mtu anaweza kukuacha lakini hauwezi kujiacha. Hivyo basi, usiharibu mipango na ndoto zako za kujiendeleza hima kimasomo au kibiashara kwa sababu ya mtu kwa sababu ya mapenzi. Mume au mke anayestahiki ni anayekuhimiza kujiendeleza binafsi.”

Anaongeza, “Maendeleo yako binafsi yanapaswa kuja kwanza kabla ya uhusiano. Mpenzi, mume au mke anaweza kukuacha na apate mwingine lakini hauwezi kujiacha. Jijenge kwanza.”