Habari Mseto

Tusibishanie chanjo – Rais Kenyatta

October 19th, 2019 1 min read

Na WINNIE ATIENO

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kuunga mkono mpango wa chanjo ya saratani ya njia ya uzazi ambayo alizindua rasmi hapo Ijumaa huku wakuu wa Kanisa Katoliki wakiitaka serikali kutathmini madhara yake kwa umma.

Rais Kenyatta alisema wasichana 800,000 watapokea chanjo hiyo katika hospitali zote za umma, zile za binafsi na za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.

Wakuu wa Tume ya Afya ya Kanisa Katoliki wakiongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mombasa, Martin Kivuva alisema chanjo hiyo ilikumbwa na utata hapo mwanzoni.

Alisema kitengo cha afya katika kanisa hilo kinataka hakikisho kuwa chanjo hiyo haina madhara.

Hata hivyo, Askofu huyo alisema saratani ni changamoto kuu nchini akipigia debe chanjo hiyo.

Lakini Rais aliwasihi Wakenya waache kulumbana kuhusiana na chanjo hiyo.

“Tafadhali tusipinge sayansi, tufanye kazi pamoja tukubaliane manake sote twawatakia watoto wetu maisha mema,” alisema Rais.