MNAMO mwaka wa 2018, serikali ya Kenya ilianza kutekeleza mpango wa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum katika jamii, maarufu kama Inua Jamii, kupitia ruzuku ya Sh2,000 kila mwezi.
Chini ya mpango huo, serikali kuu pia iliahidi kugharimia huduma za matibabu kwa wakongwe, wenye umri wa miaka 70, kwenda juu, kupitia Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF).
Lakini tangu wakati huo wakongwe waliopewa kadi za NHIF hawajaweza kupata huduma za afya katika hospitali mbalimbali kwani serikali haijatuma pesa za hazina hiyo.
Serikali isije ikasahau kuwa zaidi ya wakongwe 523,000 ambao 2018 walisajiliwa kwa mpango huu wa afya bila malipo bado wanateseka kwani wengi wao hawawezi kumudu gharama ya matibabu.