Habari MsetoSiasa

Tusipohusishwa tutasambaratisha mradi wa makaa, viongozi na wakazi watisha

July 31st, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

VIONGOZI na wakazi wa eneo kunakonuiwa kujengwa mradi wa nishati ya makaa ya mawe kaunti ya Lamu wametisha kulemaza shughuli za mradi huo endapo hawatahusishwa kikamilifu katika shughuli zinazoambatana na mradi huo.

Mradi huo wa gharama ya Sh 200 bilioni unanuiwa kujengwa katika kijiji cha Kwasasi, tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu.

Mradi huo uko chini ya udhamini wa kampuni ya Amu Power na unatarajiwa kuzalisha megawati 1,050 za umeme punde utakapokamilika.

Kufikia sasa jumla ya ekari 975 za ardhi tayari zimetengwa eneo la Kwasasi ili kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho.

Wakazi wakiongozwa na Mwakilishi wa Wadi ya Hindi, Anab Haji, wanadai tangu azma ya kuanzishwa kwa mradi eneo lao kutangazwa, mwekezaji hawajakuwa akiwahusisha wenyeji.

Mwakilishi wa wadi ya Hindi, Anab Haji. Ametisha kulemaza shughuli za mradi wa nishati ya makaa kwa kukosa kushirikishwa pamoja na watu wake. PICHA/KALUME KAZUNGU

Akizungumza wakati wa kikao na wadau mbalimbali kwenye ukumbi wa Huduma Centre mjini Lamu, Bi Haji alisema ni vyema mwekezaji kuheshimu haki za wakazi kwa kuhakikisha wamehusishwa katika kila hatua inayoambatana na mradi huo.

“Mimi ni kiongozi ambaye nimechaguliwa kuwakilisha watu wangu wa Hindi ambako mradi wa nishati ya makaa unalengwa kujengwa. Cha ajabu ni kwamba sijahusishwa kivyovyote kuhusu shughuli za mradi. Watu wangu pia hawajashirikishwa. Hii inamaanisha mwekezaji anatudharau sisi viongozi na watu wetu. Lazima tuhusishwe la sivyo hatutakubali chochote kinachoambatana na mradi huo kuendelezwa eneo letu,” akasema Bi Haji.

Naye Bw William Mwangi alisema ipo haja ya serikali na mwekezaji kutoa hamasa kwa wakazi kuhusiana na mradi huo.

“Tunaambiwa mradi una sumu lakini hata hatujaelimishwa mradi wenyewe wahusu nini. Tunahitaji hasama kutoka kwa serikali ili kujua iwapo tutapinga au kuunga mkono mradi,” akasema Bw Mwangi.

Mradi wa nishati ya makaa ya mawe umekuwa ukipokea pingamizi chungu nzima kutoka kwa mashirika ya kijamii yakiongozwa na muungano wa Save Lamu, ambayo yamekuwa yakidai kuwa mradi huo ni sumu na hatari kwa afya ya wakazi na mazingira.