Michezo

Tusiyenge asajiliwa na APR ya Rwanda

September 18th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Rwanda APR FC jana walitangaza na kumtambulisha rasmi mshambulizi wa zamani wa Gor Mahia Jacques Tuyisenge kama mchezaji wao.

Mwanadimba huyo ambaye alivuma sana enzi zake akiwa K’Ogalo, alitia saini kandarasi ya miaka miwili na APR baada ya kuagana na Petro de Atletico ya Angola.

“Tunafurahi sana kutwaa huduma wa mshambulizi Jacques Tuyisenge ambaye atatusakatia kwa kipindi cha miaka miwili kinachokuja. Tuyisenge ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi) ana uzoefu na tajriba ya kusaidia timu hii kutetea taji la ligi na pia kutushindia mataji mengine. Karibu APR FC,” ikasema klabu hiyo kupitia akaunti yao ya Facebook.

Tuyisenge hajakuwa na klabu ya kuwajibikia tangu aagane na Petro de Atletico ya Angola mnamo Agosti.

Awali ishara zote zilikuwa zikionyesha kwamba angejiunga na mababe wa Zambia, Zesco United ila inaonekana aliamua kurejea kusakata kabumbu nyumbani. Kabla ya kujiunga na K’Ogalo 2016, aliongoza Police FC ya nchi hiyo kushinda taji la ligi ya Rwanda.

Tuyisenge aliondoka K’Ogalo mnamo 2019 na kuelekea Angola baada ya kusaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) mara tatu ikifuatana. (2017, 2018, 2019).

Kando na Zesco United, iliaminika kwamba Simba SC, Yanga SC na Azam FC zote za Tanzania zilikuwa zikihemea huduma za mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28.

Naibu huyo wa nahodha wa Amavubi Stars aliondoka Petro de Atletico mwaka moja tu baada ya kujiunga nao.

“Nashukuru sana kwa kutokuwa na nafasi ya kuchezea Petro de Atletico na ni muda ambao nimeuenzi sana. Nawatakieni lila la kheri kwenye safari hii ya soka,” akasema wakati huo.

Baada ya kuondoka Angola, mashabiki wa K’Ogalo waliomba uongozi wa timu hiyo umrejeshe kikosini lakini juhudi hizo hazikufua dafu.