Tusker FC yaanza kunusia Sh60 milioni Klabu Bingwa Afrika baada ya kubandua Arta Solar

Tusker FC yaanza kunusia Sh60 milioni Klabu Bingwa Afrika baada ya kubandua Arta Solar

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa soka nchini Kenya, Tusker walipiga hatua kubwa kukaribia tuzo ya kuingia mechi za makundi ya Klabu Bingwa Afrika ya Sh60,610,000 baada ya kubandua Arta Solar 7 kwa jumla ya mabao 4-1 jijini Nairobi, Jumamosi.

Vijana wa kocha Robert Matano walijikatia tiketi ya kupepetana na miamba Zamalek kutoka Misri katika raundi ya pili baada ya kulipua mabingwa hao wa Djibouti 3-0 katika mechi ya marudiano ugani Nyayo.

Walikuwa wamelazimisha sare ya 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Septemba 11 jijini Djibouti.Hapo Jumamosi, Wanamvinyo hao walipata mabao mawili katika kipindi cha kwanza kupitia Shami Kibwana aliyefuma wavuni penalti iliyopatikana Mtanzania Ibrahim Joshua alipoangushwa ndani ya kisanduku na kichwa cha Ibrahim Joshua kutokana na krosi ya Jackson Macharia.

Mganda Deogratius Ojok, ambaye alijaza nafasi ya Joshua mapema katika kipindi cha pili, alihitimisha ufungaji wa mabao kutokana na krosi ya Macharia.Tusker sasa lazima ibandue Zamalek mwezi ujao kati ya Oktoba 15 na Oktoba 23 ndiposa ijihakikishie tuzo hiyo ya mamilioni ya fedha.

Vijana wa Matano wana rekodi duni dhidi ya wapinzani kutoka Misri kwa hivyo watalazimika kupiga kufa-kupona kupata tiketi ya mechi za makundi. Mara ya mwisho klabu hizi zilikutana ilikuwa mwaka 2005 wakati Tusker ilipoteza dhidi ya Zamalek nyumbani 1-0 na ugenini 3-1 ikiaga mashindano kwa jumla ya mabao 4-1.

Pia, ililemea na mabingwa Al Ahly kutoka Misri 5-0 mwaka 2006 na 4-1 mwaka 2013 ambao ulikuwa wake wa mwisho kushiriki mashindano haya kabla ya kurejea msimu huu wa 2021-2022.

  • Tags

You can share this post!

CBC: Onyo wazazi wasifanyie watoto kazi za ziada

Mane afikisha mabao 100 akivalia jezi za Liverpool