Michezo

Tusker na Ulinzi wakosa kufungua mifereji yao ya fedha kwa minajili ya uhamisho wa wanasoka muhula huu wa 2020

November 8th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 12 Tusker FC na wafalme mara nne Ulinzi Stars ndivyo vikosi vilivyojishughulisha kwa kiwango cha chini zaidi katika soko la uhamisho wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL) muhula huu.

Klabu hizo hazikutumia kiasi kikubwa cha fedha katika kipindi cha uhamisho kilichofunguliwa Agosti 1 na kutamatika rasmi mnamo Novemba 6, 2020.

Japo kipindi hicho cha uhamisho kilirefushwa kwa siku sita zaidi, wanajeshi wa Ulinzi Stars walisajili wanasoka watatu pekee na wakafaulu kudumisha wachezaji wote waliowachezea katika msimu wa 2019-20.

Kwa upande wao, Tusker ya kocha Robert Matano ilijinasia wachezaji wanne pekee baada ya kupoteza masogora watatu akiwemo mshambuliaji Timothy Otieno aliyetua Zambia kucheza Napsa Stars.

Wachezaji wapya waliojiunga na Ulinzi Stars ni Hamisi Abadalla (Water Works FC), Oliver Rutto (Water Works FC) na Michael Onyango (Kahawa United FC) huku Tusker ikijitwalia Jimmy Ndungi (Tusker Youth FC), Wellington Ochieng (Gor Mahia FC), Christopher Oruchum (AFC Leopards) na Kevin Monyi (Western Stima).

Mbali na Otieno, wanasoka wengine waliobanduka Tusker ni Gabriel Wandera aliyeyoyomea Nzoia Sugar FC na Peter Ngugi ambaye bado hajapata hifadhi mpya.

Hali ya Ulinzi Stars na Tusker ilikuwa tofauti kabisa na ya mabingwa watetezi na wafalme mara 19 wa Ligi Kuu ya KPL Gor Mahia ambao walijitwalia wanasoka 17 wakiwemo Andrew Juma (Mathare United), Tito Okello (Vipers SC, Uganda), Bertrand Nkofor (Al Mudhaibi FC, Oman), Jules Ulimwengu (Rayon Sports SC, Rwanda), John Macharia (FC Guria Lanchkuti, Georgia), Andrew Malisero (Commercial FC) na Samuel Njau (Western Stima).

Sajili wapya wengine kambini mwa Gor Mahia ni Benson Omalla (Western Stima), John Ochieng (Chemelil Sugar), Frank Odhiambo (Bongonaya FC), Gad Mathews (Kisumu All-Stars), Kennedy Odhiambo (Western Stima), Levis Opiyo (Nairobi City Stars), Dickson Raila (Masawa), Sydney Wahongo (Western Stima) na Kelvin Wesonga (Western Stima).

Gor Mahia pia waliagana rasmi na wachezaji 15 wakiwemo beki raia wa Uganda Shafiq Batambuze, Lawrence Juma (Sofapaka), Joash Onyango (Simba SC, Tanzania), Wellington Ochieng (Tusker), Elvis Ronack (Nzoia Sugar), Kennedy Otieno (Western Stima), Boniface Omondi (Wazito) na David Mapigano (Azam FC, Tanzania).

Wengine ni Dickson Ambundo (Dodoma Jiji FC, Tanzania), Juma Balinya (KCCA FC, Uganda), Clinton Okoth (Wazito), Fredrick Odhiambo (Wazito FC), Alphonse Omija (Kariobangi Sharks), Edwin Lavatsa na Jackson Owusu ambaye ni raia wa Ghana.

AFC Leopards ambao wanapania kukomesha kiu ya miaka 21 bila taji la Ligi Kuu ya Kenya pia walisajili wachezaji 13 wakiwemo Harrison Mwendwa (Kariobangi Sharks), John Oyemba, Peter Thiong’o (Kakamega Homeboyz), Caleb Olilo (Nairobi Stima), Washington Munene (Wazito FC), Yusuf Mainge (FK Porohnie, Slovakia).

Wengine ni Sellasie Otieno (Liberty Sports Academy), Lewis Bandi (Hakati Sportiff), Fabrice Mugheni (Rayon Sports, Rwanda), Alexandre Kouame (Kalighat Milan Sangha FC, India), Gideon Waja (Toronto II, Canada), Duncan Otieno (Nkana FC, Zambia) na Bienvenue Shaka (Etoile Du Sahel, Tunisia).

Wakati uo huo, Leopards waliagana na wanasoka tisa wakiwemo Dan Musamali (Nzoia Sugar), Daniel Kakai (Zoo FC), Vincent Oburu (Wazito), Christopher Oruchum (Tusker), Maxwel Mulili (Zoo FC), Francis Manoa, Vincent Wonder Odongo, Luis Tera na Clark Achuka.

Vihiga United waliofuzu kwa gozi la Ligi Kuu ya Kenya msimu ujao wa 2020-21 baada ya kupiga Kisumu All-Stars 5-3 kupitia penalti hawakujumuishwa kwenye orodha hiyo ya uhamisho wa wachezaji iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).