Michezo

Tusker sasa yainuka Gor na Ingwe wakijikwaa Ligi Kuu

February 11th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa zamani Tusker, Sofapaka na Mathare United wameimarika kwenye jedwali la Ligi Kuu ambayo imeshuhudia mabadiliko 10 baada ya mechi za raundi ya 21 kusakatwa wikendi.

Tusker ilikuwa timu ya pekee ndani ya mduara wa saba-bora iliyozoa ushindi wikendi. Imerukia nafasi ya pili baada ya kukifisha alama 38 kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AFC Leopards mnamo Jumapili.

Wanamvinyo hao, ambao walikuwa alama sita nyuma ya Gor Mahia kabla ya ushindi huo, sasa wamepunguza uongozi wa vijana hao wa Steven Polack hadi alama tatu.

Mabingwa watetezi Gor walisalia kileleni kwa alama 44 baada ya mechi yao ya 19 kuishia kwa kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Sofapaka.

Kakamega Homeboyz iko sako kwa bako na Tusker kwa alama 41, ingawa imeteremka nafasi moja hadi nambari tatu kwa tofauti ya ubora wa magoli baada ya kukabwa 1-1 dhidi ya Bandari.

Wanabenki wa KCB pia wameshuka nafasi moja hadi nambari nne. Walizabwa 1-0 na Kariobangi Sharks na kusalia na alama 38.

Wanajeshi wa Ulinzi Stars hawajasonga kutoka nafasi ya tano, ingawa waliimarisha alama zao hadi 36 baada ya kuokota alama moja katika sare ya 1-1 dhidi ya Nzoia Sugar.

Leopards inabaki katika nafasi ya sita kwa alama 34 baada ya kupoteza penalti ikilemewa na 1-0 na Tusker uwanjani Afraha mjini Nakuru.

Western Stima, ambayo imeambulia alama moja kutoka mechi nne zilizopita baada ya kuchapwa 2-1 na Wazito, imekwamilia nafasi ya saba kwa jumla ya alama 31.

Sofapaka na Mathare zimepaa nafasi moja kila mmoja na kutulia katika nafasi ya nane na tisa kwa alama 30 na 29, mtawalia. Batoto ba Mungu walikung’uta Gor 3-1 nao Mathare ikipatia Zoo dozi sawa na hiyo.

Posta Rangers inakamilisha timu 10 za kwanza baada ya kuduwazwa 2-1 na Chemelil Sugar na kusalia na alama 29. Rangers iko nyuma ya Mathare kwa tofauti ya ubora wa magoli.

Bandari inashikilia nafasi ya 11 kwa alama 20 baada ya kukamilisha mechi yake ya tano bila ushindi ilipokabwa 1-1 na Homeboyz uwanjani Mbaraki.

Sharks ni ya 12 kwa alama 19 baada ya kuandikisha ushindi wake wa pili mfululizo ilipozima KCB, ambayo haikuwa imepoteza mechi tisa mfululizo.

Ushindi wa kwanza wa Wazito katika mechi tisa, ulitosha kuisukuma juu nafasi moja hadi nambari 13. Wazito imevuna alama 15. Iko mbele ya nambari 14 Zoo kwa tofauti ya ubora wa magoli.

Zoo imeambulia alama mbili katika mechi nane zilizopita. Nzoia imesalia katika nafasi ya 15 kwa alama 12.

Na kwa mara ya kwanza msimu huu, Chemelil Sugar imetoka mkiani. Ilichapa Rangers na kurukia nafasi ya 16. Ina alama tisa, moja zaidi ya Kisumu, ambayo inavuta mkia baada ya kuteremka nafasi moja. Kisumu imepoteza mechi 10 zilizopita.