Michezo

Tusker yaponea kichapo cha Rangers

June 12th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BONIFACE Muchiri alinasua Tusker FC kutoka minyororo ya kudondosha alama zote tatu katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Posta Rangers iliyomalizika 2-2 uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi, Jumatatu.

Tusker ya kocha Robert Matano ilitangulia kuona lango kupitia shuti kali kutoka kwa mshambuliaji Michael Khamati dakika ya 30.

Hata hivyo, Gearson Likonoh alisawazishia Rangers dakika ya 55 kupitia frikiki safi ambayo kipa Duncan Ochieng’ hakufaulu kupangua.

Rangers iliongeza bao la pili dakika ya 78 kupitia Jeremiah Wanjala. Dennis Mukaisi alifanya kazi nzuri ya kumchenga Llyod Wahome kabla ya kuvuta shuti kali lililokamilishwa na Wanjala. Tusker iligawana alama na Rangers baada ya Muchiri kukamilisha mpira mzuri kutoka kwa kichwa cha Peter Nzuki dakika ya 88.

Nambari tisa Rangers, ambayo haijapoteza dhidi ya Tusker, sasa ina jumla ya alama 24 kutokana na ushindi tano, sare tisa na vichapo vinne. Mabingwa mara 11 Tusker wako alama moja nyuma katika nafasi ya 11 kutokana na ushindi sita, sare tano na vipigo vinane.