HabariSiasa

Tutafagia wafisadi wote, aapa Uhuru

December 13th, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano aliapa kuwaadhibu maafisa wakuu serikalini wanaoshiriki ufisadi akisema hatalegeza kamba licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya wanasiasa.

Rais Kenyata pia alitangaza kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya, waharibifu wa mazingira na walaghai wanaohepa kulipa ushuru katika kipindi chake kilichosalia.

Alionya kuwa watumishi wa serikali wanaotumia afisi zao vibaya kwa kuhangaisha wananchi na hata kuomba rushwa watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Rais alisema vita dhidi ya ufisadi vimeanza kuzaa matunda, “kwa kuwa maafisa wakuu serikalini waliodhani hawawezi kuguswa na yeyote tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi.”

“Wezi wa fedha za umma na watumishi wa serikali wanaotumia vibaya mamlaka, mnaweza kukimbia lakini hamtakuwa na pahala pa kujificha. Mtalipa kila shilingi mliyopora,” akasema Rais.

Akihutubia taifa jana wakati wa maadhimisho ya miaka 55 tangu Kenya ijipatie uhuru, Rais alisema serikali yake imeanza mikakati ya kunasa walanguzi wa dawa za kulevya.

“Serikali inashirikiana na maafisa wa ujasusi kutoka mataifa ya kigeni kunasa walanguzi wa watoto na dawa za kulevya. Hatutaruhusu Kenya kuwa soko la mihadarati na maficho ya walanguzi,” akasema Rais.

Kiongozi wa nchi pia aliwataka Wakenya wote kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa nchi.

Rais alitoa kauli hiyo siku chache baada ya viongozi kutoka eneo la Bonde la Ufa, wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei kudai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga watu wa jamii ya eneo hilo.

Kulingana na Bw Cherargei, vita hivyo vinanuia kutatiza ndoto ya naibu wa Rais William Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022.

“Hatutatimiza malengo yetu ya kuwa na Kenya bora tusipoungana na kushinda zimwi la ufisadi. Hii ndiyo maana tumeimarisha juhudi za kukabiliana na ufisadi,” akasema.

Alisema serikali imetia saini mikataba na mataifa mbalimbali kama vile Uswizi, Uingereza na Kisiwa cha Jersey kuhakikisha fedha zilizofichwa katika nchi hizo na wafisadi zinarejeshwa nchini.

Rais Kenyatta kwa mara nyingine aliishambulia Idara ya Mahakama kwa kuwaachilia huru washukiwa wa ufisadi kwa dhamana ya kiasi kidogo cha fedha.

Rais Kenyatta aliilimbikizia lawama Idara ya Mahakama inayoongozwa na Jaji Mkuu David Maraga kwa kujikokota katika kushughulikia kesi za ufisadi hivyo “kuchelewesha haki”.

“Nakubali kwamba washukiwa wanahitaji kusikizwa na kutendewa haki. Lakini Mahakama inastahili kuhakikisha haitumiwi na washukiwa wa wizi wa mali ya umma kukwepa mkono wa sheria,” akasema Rais Kenyatta.

“Wakenya wanakata tamaa wanaposhuhudia mahakama ikiwaachilia huru washukiwa wa ufisadi kwa dhamana hafifu. Hiyo ni sawa na kuchelewesha haki,” akaongezea.

Rais Kenyatta alielezea masikitiko yake siku moja baada ya mahakama kuachilia huru maafisa wakuu wa Hazina ya Bima ya Matibabu (NHIF), akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Geoffrey Mwangi na Meneja wa Fedha Simon Kirgotty, wanaokabiliwa na mashtaka ya wizi wa Sh1.1 bilioni, kwa dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja.

Washukiwa wengine ambao ni maafisa wa ngazi za chini, akiwemo afisa wa bodi ya kutoa kandarasi Fredrick Sagwe anayedaiwa kuwa tajiri kupindukia, waliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000.