Habari za Kitaifa

Itabidi tufinye hapa Mswada wa Fedha ukikataliwa, asema Waziri Ndung’u


HAZINA ya Taifa imetahadharisha Bunge kuwa iwapo mapendekezo ya kuongeza mapato ya serikali yaliyo katika Mswada wa Fedha wa 2024 hayatapitishwa, nchi inaweza kukabiliwa na upungufu wa mapato ya Sh200 bilioni mwaka wa kifedha wa 2024-25.

Katika barua kwa karani wa Bunge Bw Samuel Njoroge, aliyoandika Jumatano Juni 19, Waziri wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u, anasema kuwa kutakuwa na marekebisho kwa matumizi, ambayo yataathiri idara mbalimbali za Serikali.

Serikali itahitaji kurekebisha matumizi yake na kupunguza mgao kwa baadhi ya idara za serikali ambazo kuna uwezekano wa kuongezeka kwa madeni ambayo hayajalipwa iwapo mapendekezo ya kuongeza ushuru hayatapitishwa.

Baadhi ya taasisi zitakazokabiliwa na tishio la kupunguziwa bajeti ni pamoja na Wizara ya Elimu ya Msingi (Sh3.4 bilioni), Idara ya Huduma za Matibabu (Sh4.7 bilioni), Idara ya Barabara (Sh15.1 bilioni), Kilimo (Sh6.7 bilioni) Idara ya Ulinzi wa Jamii (Sh5.5 bilioni) na Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) (Sh18.9 bilioni).

Prof Ndung’u aliorodhesha angalau afisi 45 za serikali, Mahakama, na Bunge ambazo zitapunguziwa bajeti iwapo bunge litakosa kupitisha mswada huo.

Waziri huyo alisema iwapo Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2024 utaidhinishwa ilivyopendekezwa na Hazina ya Kitaifa kwa nia ya kukusanya Sh302 bilioni, Bunge linaweza kuendelea na kuzingatia Mswada wa Matumizi ya Fedha wa 2024 uliowasilishwa Bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza.

“Hata hivyo, ikiwa hatua za kuongeza mapato zilizo katika Mswada wa Fedha wa 2024 hazitapitishwa na Bunge, kuna uwezekano wa kuwa na upungufu wa mapato wa takriban Sh200 bilioni. Hii inamaanisha matumizi ya jumla yatapungua katika mihimili mitatu ya Serikali,” akasema Prof Ndung’u.

Waziri alidokeza kuwa atawasilisha hatua za ziada kwa Bunge kufikia kesho Juni 21, ili kufidia salio la Sh21.6 bilioni.

Mbali na Idara za Serikali zilizoorodheshwa, Waziri huyo alibainisha kuwa zingine zitakazoathirika ni pamoja na Afisi ya Rais Sh451 milioni, Ikulu (Sh500 milioni), Masuala ya Ndani (Sh2 bilioni), Maeneo Kame na Kavu na Maendeleo ya Ukanda wa Kaskazini (Sh4.6 bilioni).

Nyingine ni pamoja na Sh7.75 bilioni za wizara ya ulinzi, Elimu ya mafunzo ya Kiufundi  (TVET) (Sh 800milioni), Masuala  ya Nje (Sh 1.85bilioni), Hazina ya Kitaifa ikiwa ni pamoja na  Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru  Kenya (KRA) na Shirika la Ndege la Kenya (KQ) (Sh12.7bilioni), Elimu ya Juu na Utafiti Sh8.3 bilioni na, maji Sh11.6 bilioni miongoni mwa nyingine.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo ameteta kuwa hakuna sababu ya tahadhari, kwa kuwa serikali bado inaweza kutumia sheria ya fedha ya 2023.