Tutafungiwa iwapo hamtatii – Mandago

Tutafungiwa iwapo hamtatii – Mandago

Na TITUS OMINDE

WAKAZI wa Kaunti ya Uasin Gishu watafungiwa ili wasitoke eneo hilo iwapo wataendelea kupuuza sheria za kukabiliana na msambao wa virusi vya corona, Gavana Jackson Mandago ameonya.

Bw Mandago alisema kadri viwango vya maambukizi vinapoendelea kuongezeka katika kaunti hiyo ndivyo kufungiwa kunavyonukia.Akihutubu mjini Eldoret, Bw Mandago aliwataka wakazi kuwajibika vilivyo na kuzingatia sheria zilizowekwa ili kukabili maambukizi hayo.

“Iwapo tutaendelea kupuuza sheria za kukabiliana na maambukizi ya corona, tujue tutalazimu serikali kuu kutufungia, jambo ambalo litaathiri uchumi wetu na maisha ya kila leo,” alisema Bw Mandago.

Bw Mandago alitaka kila mtu kuwajibika na kufuata sheria za wizara ya afya katika vita dhidi ya corona.Gavana huyo alisema kwamba baadhi ya wakazi wamechukulia suala la corona kama mzaha ambapo hawavai barakoa kama inavyohitajika.

Bw Mandago alistaajabishwa na ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo katika kaunti hiyo, huku akisema kutojali na kupuuza sheria za wizara ya afya kumechangia hali hiyo.

“Takwimu za hivi punde kuhusu maambuzi ya corona zaonyesha kuwa tuko katika hatari ya kufungiwa. Hapo jana tulikuwa na maambukizi 69 katika kaunti hii. Hali hii ikiendelea huenda Rais akalazimika kufunga kaunti yetu.Hatua kama hiyo ni hatari kwa uchumi wetu,” alisema Bw Mandago.

Kiongozi huyo aliwataka wahudumu wa sekta ya uchukuzi wa umma kuzingatia sheria hizo kama hapo awali.Alisikitika kwamba wenyeji wanangojea kulazimishwa na polisi kuvaa barakoa.

“Watu wanafanya mzaha na suala zima la Corona. Kwa sasa wanavaa barakoa kama bangili, wakiona polisi ndipo huvaa barakoa. Barakoa si ya polisi bali ya kukulinda wewe,” alisema Bw Mandago.

Gavana huyo kwa sasa amewataka maafisa wa usalama kuimarisha msako dhidi ya watu wote ambao wanapuuza masharti yaliyowekwa katika vita dhidi ya virusi hivyo bila mapendeleo.

Vile vile, gavana alirejelea wito wake wa kutaka wazee wa umri wa zaidi ya miaka 58 kujiepusha na shughuli za mjini na badala yake wasalie nyumbani ili kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Matamshi ya gavana Mandago yaliungwa mkono na viongozi wa kidini ambao walisema wakazi wa kaunti hiyo wameanza kuchukulia suala la virusi hivyo kimzaha. Mwenyekiti wa muungano wa wahubiri kaunti hiyo askofu Wilson Kurui alisema ni kazi ya kila mtu kuwajibikia swala hilo.

“Tuheshimu na kuzingatia masharti tuliyopewa katika kukabiliana na janga hili. Viongozi wa kidini wanapaswa kuhakikisha kuwa sheria hizi zinadumishwa katika maeneo yote ya ibada,” alisisitiza askofu Kurui.

Kwa sasa, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza uamuzi wa serikali kufunga kaunti tano ambazo ni Nairobi, Nakuru, Kiambu, Machakos na Kajiado zilizokuwa na idadi kubwa ya maambukizi.

You can share this post!

JAMVI: Hivi anavyokuja Obado, ndiye kizibo cha Raila Nyanza?

Maseneta wakosoa Joho kuhusu matumizi ya feri