Habari Mseto

Tutagoma kuanzia Novemba 21 – Wauguzi

November 12th, 2018 1 min read

Na ALEX NJERU

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wauguzi Kenya (KNUN), tawi la Kaunti ya Tharaka-Nithi, Bw Fabian Marigu amesisitiza kwamba mgomo wao wa kitaifa uliopangiwa kuanza Novemba 21 hautasitishwa isipokuwa kama serikali za kaunti zitatimiza makubaliano waliyoafikiania katika mkataba wa Novemba 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Chogoria hapo jana, Bw Marigu alisema jitihada zake za kuzungumza na serikali ya Gavana Muthomi Njuki hazijazaa matuda yoyote na kwamba hawana budi kujiunga na wenzao katika mgomo huo.

“Isipokuwa serikali yetu ya kaunti itimize makubaliano ya mkataba wa Novemba 2017, wauguzi watagoma Novemba 21,” alisema Bw Marigu.

Aidha alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba licha ya uvumilivu wa wauguzi na jitihada za chama hicho kuhakikisha kwamba makubaliano hayo yametekelezwa kwa utaratibu waliokubaliana, waajiri wao wamenyamaza tu.

Aliongeza kuwa ni hatari kubwa kusitisha huduma za afya wakati wa mvua ambapo magonjwa mengi yakiwemo yale ya kipindupindu utokea lakini hawana budi kwani ndio njia pekee ya kufungua masikio ya serikali.

Katika barua iliyotumwa kwa Afisa Mkuu Mtendaji Baraza la Magavana, Katibu wa Wizara ya Afya na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Mishahara kutoka ofisi ya kitaifa ya chama cha wauguzi mnamo Novemba 7, waajiri wana siku 14 kutimiza makubaliano ya Novemba 2017.

Kwa mujibu wa mkataba huo, wauguzi walitakiwa kulipwa Sh15,000 kama posho ya sare na za hatari zinazohusiana na kazi yao kati ya Sh20,000 na Sh25,000, kulingana na kiwango cha kazi katika mwaka wa kwanza wa kifedha.

Kutiwa sahihi kwa makubaliano hayo kulisitisha mgomo uliokuwa umechukua mwezi mitano.