Michezo

Tutailiza Liverpool ugani Old Trafford, asema Ashley Young

February 21st, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MLINZI wa Manchester United Ashley Young amesema kwamba wanalenga kuonyesha Liverpool kivumbi, timu hizo zitakapochuana kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Jumapili Februari 24 ugani Old Trafford.

Young amesema kwamba timu hiyo ina hamasa na ari ya kutia breki mbio za The Reds za kufukuzia ubingwa wa EPL haswa baada ya kuangusha Chelsea kwenye mechi ya kufuzu robo fainali ya kipute cha FA.

Man United imekuwa kiazi moto kwa wapinzani tangu mkufunzi wao mpya Ole Gunar Solskjaer achukue usukani baada ya aliyekuwa kocha wao Jose Mourinho kuonyeshwa mlango mwezi Disemba mwaka wa 2018.

Chini ya usimamizi wa Ole Gunar, The Red Devils wameishinda timu kubwa kubwa kama Tottenham Hot Spur, Arsenal na Chelsea.

Kulingana na mlinzi huyo wa zamani wa Aston Villa, ushindi dhidi ya Chelsea umewapa motisha kwamba ‘hakuna lisilowezakana’ wakichapana na Liverpool.

“Ushindi dhidi ya Chelsea umetufungua macho na kutuonyesha kwamba tunaweza kutwaa ushindi dhidi ya Liverpool. Tukijiamini na kusakata gozi jinsi tulivyofanya basi hatuwezi kukosa kutamba,” akasema Young.

“Tulishinda Tottenham Hot Spur, Arsenal na Chelsea ugenini na tunaweza kuendeleza wimbi hilo la ufanisi dhidi ya timu za haiba mbele ya mashabiki wetu nyumbani tukigaragazana na Liverpool Jumapili,” akaongeza Muingereza huyo.

Iwapo Liverpool watabwagwa basi watakuwa na kibarua kigumu cha kuinyang’anya bingwa mtetezi Manchester City kombe mdomoni huku idadi za mechi zilizosalia za EPL msimu huu wa 2018/19 ikizidi kupungua.