Habari Mseto

Tutainua Msambweni, wafuasi wa Ruto waahidi

November 2nd, 2020 1 min read

Na FADHILI FREDRICK

WASHIRIKA wa Naibu Rais William Ruto wametua Msambweni kumpigia debe mgombea wa kujitegemea Feisal Bader kwenye uchaguzi mdogo wa Disemba 15 na kuahidi kuwa mabadilko ya maana yataanza kuonekana eneo hilo.

Wakiongozwa na Maseneta wa zamani Johnstone Muthama, Boni Khalwale na Hassan Omar, walisema uchaguzi huo mdogo ndio utakuwa mwanzo wa mabadiliko halisi ya kisiasa nchini.

Akizungumza katika kijiji cha Mafisini kwenye mkutano wa kisiasa, Bw Omar alisema ni wakati wa mageuzi ambayo yateletwa na Wakenya wa kawaida.

Alisema ana matumaini haya yatatimizwa na wakazi wa Msambweni watakaomchagua Bw Bader kwani yeye ni mtu wa chini ambaye anajali na kutilia maanani maisha ya wananchi.

“Tumechoshwa na siasa za urithi ambapo wananchi wa kawaida hawana nafasi ya kuongoza lakini sasa mambo yatabadilika kwa kuwachagua viongozi wa tabaka la chini kuongoza taifa hili,” akasema.

Bw Omar alisema uchaguzi huo sio tu wa wagombeaji bali utadhihirisha mwongozo wa siasa za 2022.

“Tunasisitiza wito wa hasla kama kauli mbiu yetu ya kuchagua watu kutoka tabaka la chini ili kuwezesha kila mtu kupata fursa sawa nchini,” akasema.

Bw Khalwale alisema uchaguzi huo mdogo ni safari ya kuwakomboa watu wa tabaka la chini akiongeza kuwa, siyo viongozi wa tabaka la juu ambao wazazi wao wametawala nchi wanaweza kuongoza nchi hii.

Alisema Kenya ina watu wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kuongoza na kuliendeleza taifa hili kimaendeleo.

“Hatutakubali kutawaliwa na viongozi wabinafsi na walafi lakini tunataka nchi ambayo watu kama Bader kutoka tabaka la chini wanaweza kushikilia nafasi za kuongoza nchi,” alisema, akiwataka watu wasiyumbishwe na joto la siasa na kushindwa kumchagua kiongozi atakayejali masilahi yao.

Bw Khalwale alimiminia sifa tele Bw Bader, akisema ni mwenye uzoefu na amefanya kazi na marehemu Dori na ndiye atakayeendeleza miradi ilioanzishwa na marehemu.