Michezo

Tutajinyanyua msimu ujao, wasema South B United

June 24th, 2020 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

BAADA ya timu ya South B United kuteleza mara mbili kwenye mbio za kupigania ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom bado imepania kubeba taji la kitaifa msimu ujao.

Kando na hayo wachezaji hao walikuwa kati ya vikosi 22 vilivyokuwa vikishiriki migarazano ya taji la Nairobi West Regional League (NWRL) kabla ya kusitishwa na mlipuko wa virusi hatari vya corona muhula wa 2019-20. Ingawa haikuwa imekaa vizuri kwenye jedwali la michuano hiyo ilikuwa kati ya vikosi saba bora.

South B United inashiriki michezo ya mashinani lakini inajivunia kukuza chipukizi kadhaa ambao husakatia klabu za Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL), Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza na Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

Kocha wake, John Mandela anasema ”Licha ya kuyumbishwa na mtindo wa kila msimu kupoteza baadhi ya wachezaji wazuri tunalenga kukaza buti tuhakikishe tunatwaa tiketi ya kushiriki Ligi Kuu ya KPL ndani ya miaka mitatu au minne ijayo.”

CHAPA DIMBA NA SAFARICOM

Anaamini kuwa wachezaji wake wanatosha mboga kufanya kweli kwenye kampeni za kufukuzia tiketi ya kushiriki kipute cha haiba ya juu nchini.

”Bado hatujayeyusha matumaini ya kubeba ubingwa wa kitaifa kwenye mikwaruzano ya Chapa Dimba na Safaricom.”

”Tunalenga kuanza maandalizi ya mapema kwenye juhudi za kujiweka imara kushiriki ngarambe hiyo makala ya nne baada ya janga la virusi hatari vya corona kudhibitiwa.”

Ndani ya makala mawili ya michuano hiyo South B United inajivunia kushiriki mara moja fainali katika kitaifa zilizoandaliwa Kinoru Stadium, Kaunti ya Meru ilikobanduliwa katika nusu fainali mapema mwaka uliyopita.

South B ilishiriki fainali hizo baada ya kuibuka mabingwa wa Mkoa wa Nairobi kwa kuduwaza Jericho Allstars mabao 2-1. Katika nusu fainali ilinyuka Uweza FC mabao 2-0 nayo Jericho Allstars ilizoa 2-1 dhidi ya Brightstar Academy.

Kadhalika katika mechi za Shirikisho la Soka la Nairobi (FKF) Tawi la Nairobi West (Magharibi) ilinyamazisha Vapor Sports kwa mabao 5-4 kupitia mipigo ya matuta.

Kwenye kipute hicho mwaka huu ilibanduliwa katika fainali za Mkoa wa Nairobi na kukosa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa zinazoratibiwa kupigwa baada ya mkurupuko wa corona kudhibitiwa.

UHISPANIA

Klabu hiyo imelea Ibrahim Dawo aliyesafiri nchini Uhispania kwa majaribio ya kusakatia klabu moja katika taifa hilo. Inajivunia wengine ambao huchezea vikosi tofauti humu nchini wakiwamo: Stephen Oduor na Alvin Odoyo wote Migori Youth zote BNSL. Stephen Oduor, Brian Ngolyo, Kepha Wanjala, Enock Wanyama na Bakari Hussein wote Ligi Ndogo (Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza). Pia wapo: Jimmy Wafula na Mohammed Abdi Razak (Kibera United), Karani Clifford na Boniface Mwirigi (South B Sportiff) zote Ligi ya Taifa Daraja la Pili.