Habari MsetoSiasa

Tutakufa na Ruto liwe liwalo, Dori na Jumwa wasisitiza

December 19th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WABUNGE walioasi chama cha ODM eneo la Pwani, wamesema wako tayari kupoteza viti vyao na uongozi kwa jumla iwapo kumuunga mkono na kumpigia debe Naibu wa Rais William Ruto ili kutwaa uongozi wa nchi hii ifikapo 2022 ni makosa.

Mnamo Jumanne, viongozi hao waliandamana na Bw Ruto katika ziara ya siku moja kaunti ya Lamu, ambako Bw Ruto aliongoza hafla ya kufungua rasmi Shule ya Upili ya Wasichana na Pate kabla ya kufululiza hadi Mpeketoni ambako aliongoza hafla ya mchango.

Wakihutubia umma katika kisiwa cha Pate, Wabunge hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa Pwani ambaye pia ni Mbunge wa Msambweni, Bw Suleiman Dori, walisema wataendelea kutembea kwa pamoja katika safari ya kumpigia debe Bw Ruto wanayedai tayari ameonyesha dalili za kuwafaa watu wa Pwani.

Bw Dori aliwataka viongozi na wakazi wa Pwani kuungana ili kufanikisha azma ya Bw Ruto kufikia 2022.

“Leo tuko hapa Pate ili kuonyesha umoja wetu na safari yetu ya pamoja na Naibu wetu wa Rais, William Ruto. Yeye ameonyesha wazi kwamba anawapenda wapwani na yuko tayari kusuluhisha matatizo ambayo yametusumbua hapa Pwani miaka yote. Ningewasihi kutoyumbishwa na mtu yeyote. Wachaneni na masuala yanayaoangaziwa kwenye vyombo vya habari eti Dori yuko hivi au Aisha Jumwa yuko vile. Wacha niwaeleze wazi kwamba sisi tuko tayari kupoteza viti vyetu au uanachama wetu iwapo kumuunga mkono na kufanya kazi na Bw Rutyo ni makosa,” akasema Bw Dori.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa alisema wakazi wa Pwani wamechoka kwa kuishi katika taabu na mateso kwa muda mrefu.

Bi Jumwa alisema wakati umewadia kwa wapwani kuamka na kumchagua kiongozi anayewajali.

Mbunge huyo aidha amepinga vikali pendekezo kwamba baadhi ya maeneobunge na kaunti kuvunjiliwa mbali ilhali nyingine zikiunganishwa.

“Kama ni mateso tumeyaona. Dhiki tumepata hasa sisi Wapwani. Kusema kweli wanaosema kaunti za Lamu na Tana River zivunjiliwe mbali kamwe hawatupendi. Hiyo ni hatua ya kuturudisha nyuma. Msimamo wetu ni kwamba kaunti zote 47 zibakie zilivyo. Ninajua kwamba hayo yote yanafanywa ili kuunda nafasi tatu kuu za serikali. Hatutakubali. Tutaendelea kuchapa kazi na Bw Ruto ili aweze kuongoza nchi hii. Haturudi nyuma,” akasema Bi Jumwa.