Makala

Tutakusaidia kupata mke, Maribe amwambia Itumbi

March 19th, 2024 1 min read

ELIZABETH NGIGI na CHARLES WASONGA

MWANAHABARI Jacque Maribe amevunja kimya chake kuhusu uvumi unaoenekezwa kuhusu uhusiano wake na mwanamkakati wa kidijitali Dennis Itumbi.

Kwenye ujumbe kwa Itumbi anapoadhimisha Siku yake ya Kuzaliwa, Maribe alisema yeye na marafiki wengine wa afisa huyo watamtafutia mke mwaka huu (2024), “kwa hivyo watu wakome kudhani kuwa ni mimi.”

“Heri njema siku ya kuzaliwa Dennis Itumbi. Miongo miwili ya urafiki imedhihirishwa na pandashuka na upendo. Huu mwaka mpya, kundi hili kwenye picha litakutafutia mke, kwa hivyo watu wakome kudhani ni mimi,” Maribe akaandika kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Hii sio mara ya kwanza kwa uhusiano kati ya Maribe na Itumbi kuzua gumzo na uvumi wa uwepo wa mahaba kati yao.

Januari 2024, Maribe kwa mzaha alimjulisha Itumbi kama mkaza mwana wa babake katika stori fulani katika mtandao wa Instagram.

Aliandamanisha stori hiyo na picha ya Itumbi akiwa na babake.

“Bw Maribe na mkaza mwana wake, bila kujali yale ambayo kila mtu anasema, tunasalia familia moja,” Jacque akasema, na hivyo kuibua uvumi kwamba yeye na Itumbi ni wapenzi.

Kabla ya hapo, Itumbi aliwahi kumshangaza Bi Maribe kwa kumpa shada la maua akiwa studioni siku moja mwanahabari huyo alipokuwa akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake.

Kabla kuondoka hewani, Bi Maribe alikuwa akihudumu kama mwanahabari wa runinga ya Citizen inayomilikiwa na Shirika la Habari la Royal Media Services (RMS).

Uhusiano wao uliendelea kudhihirika mnamo Januari 2024 wakati Itumbi alielezea furaha yake baada ya Maribe kuondolewa lawama kuhusiana na tuhuma za kushirikia mauaji ya Monica Kimani.

Itumbi, ambaye alisimama kando ya Maribe muda wote uamuzi huo ukisomwa, aliutaja kama uliofichua ukweli na kuondoa uwongo.

Bw Itumbi akasema: “Imekuwa ni miaka sita, safari kwenye kivuli, ambako minyororo ya uwongo ililenga kufunga rafiki yangu ninayemthamini zaidi.”

Mnamo Jumatatu, Machi 18, 2024, Bw Itumbi aliadhimisha miaka 39 tangu kuzaliwa kwake.