Kimataifa

Tutamtupa Diamond ndani maisha akitumbuiza Wakenya, yasema TZ

December 20th, 2018 1 min read

NA RICHARD MAOSI

Msanii wa Bongo Flava Diamond Platinmz atapata kifungo cha maisha endapo atawatumbuiza mashabiki wake nchini Kenya. Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) lilithibitisha hayo Jumatano.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa BASATA Bw Onesmo Kayanda, Diamond atashtakiwa kwa kosa la uhaini ikiwa atawatumbuiza mashabiki wake nchini Kenya katika shoo kubwa ambayo imeratibiwa kufanyika katika mji wa Embu, Mombasa na Nairobi.

“Hana budi ila kufuata matakwa ya BASATA,lau sivyo hataponyoka mkono mrefu wa sheria kwa kupata kifungo cha maisha,” Bw Onesmo alisema.

Iwapo atakaidi agizo la Baraza la sanaa Diamond atafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Wasafi Classic inayomilikiwa na msanii Diamond kwa upande mmoja wamepuzilia madai hayo wakisema hafla hiyo itaendelea kama ilivyopangwa, mikakati ikiwekwa na wasimamizi wa Wasafi kutafuta mwafaka na serikali.

Kulingana na BASATA, Diamond amekuwa akisababisha vurugu katika tamasha zake nyingi na kupatia polisi wakati mgumu.

Aidha BASATA wamepinga ombi la Diamond kutumbuiza mashabiki ndani ya nchi ya Tanzania.

Majuzi Diamond alijikuta taabani baada ya kucheza wimbo wa Mwanza uliokuwa umepigwa marufuku kwa kuonesha picha chafu.

“Alitakiwa kulipa faini ya 400,000 lakini mpaka sasa hajafanya hivyo,” Bw Onesmo aliongeza.

Aprili mwaka huu Diamond alijikuta hatiani baada ya kuanika picha mtandaoni akimbusu mwanadada fulani.

Ingawa inasemekana Diamond ameanzisha harakati za kuhama nchini Tanzania siku za hivi karibuni”Kama hawataki nicheze muziki wangu Tanzania ninaweza kuhamia Kenya sehemu ambayo sitazuliwa,”Diamond alisema.