Habari Mseto

Tutashughulikia matatizo ya wanajeshi – Omamo

December 27th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

WAZIRI wa Ulinzi, Raychelle Omamo amepongeza vikosi vya kijeshi vya Kenya kwa kazi ya kulinda taifa na kupambana na wanaotishia usalama, akivihakikishia msaada wa serikali.

Bi Omamo alisema kuwa serikali inawaza kuhusu mbinu tofauti ambazo inaweza kutumia kuwasaidia wanajeshi wakati wanapotekeleza jukumu la kulinda mipaka ya nchi, akieleza kuwa serikali inajua matatizo wanayopitia wanapokuwa kazini.

“Nimekuja hapa kuwa nanyi na kufurahia pamoja nanyi msimu huu,” akasema Bi Omamo.

Alisema kuwa alitaka kusikia matakwa yao na kuonana nao moja kwa moja, ili serikali ifahamu zaidi mahali inaweza kusaidia.

“Nyinyi ni ishara ya kila kitu chenye thamani katika taifa letu kwani mmesimama imara kama ngao ya taifa letu,” waziri huyo akasema.

Bi Omamo alisema hayo alipotembelea wanajeshi wa KDF katika maeneo ya Manda, Hulugho na Kolbiyow karibu na mpaka wa Somalia, akiandamana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Samsom Mwathethe.