Habari Mseto

Tutatokomeza corona kila mtu akitii amri – Rais

April 17th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Wanaochukulia Covid – 19 kiholela wajue si ugonjwa wa kutania kwa kuwa umetikisa mataifa yaliyoimarika kiuchumi kwa kiasi kikuu ulimwenguni, hii ndiyo kauli ya Rais Uhuru Kenyatta kwa Wakenya.

Kwenye hotuba yake mnamo Alhamisi kwa taifa, Rais Kenyatta alisema ni wajibu wa kila mwananchi kuchukua tahadhari dhidi ya Covid – 19, ugonjwa unaosababishwa na virusi hatari vya corona.

“Tumeona mataifa yaliyo tajiri karibu mara 20 kuliko nchi yetu hawakuchukua tahadhari, sasa wanazika idadi kubwa ya watu. Tusifikie hapo. Ni jukumu la kila Mkenya kujikinga, kukinga familia yake, jirani yake na Kenya kwa jumla,” akasisitiza kiongozi huyo wa nchi, bila kutaja mataifa yaliyoathirika na janga la corona.

Akipigia upatu jitihada za serikali yake kukabili virusi vya corona, Rais Kenyatta alisema mikakati iliyowekwa itafaulu ikiwa “kila Mkenya atatekeleza wajibu wake kudhibiti maenezi.”

“Tuko na shida na hii shida si yetu, tumeletewa kutoka nje. Inakumba karibu kila taifa duniani. Huu ugonjwa hauchagui tajiri wala maskini, mtoto wala mzee, tushirikiane kuukabili kwa kufuata maagizo na utaratibu uliotolewa na wizara ya afya,” Rais akahimiza.

Akikiri kuzorota kwa uchumi hapa nchini Kenya na dunia kwa jumla, Rais aidha alieleza kusikitishwa kwake na kasi ambayo wananchi wanapoteza nafasi za kazi kutokana na athari za janga la corona.

Hata hivyo, alisema huu si wakati wa kurushiana maneno na kunyoosheana kidole cha lawama, ila ni wakati wa kushirikiana kukabiliana na Covid – 19. “Tushirikiane, tupambane na hili janga ili turejeshe uchumi wetu katika hali ya kawaida tuendelee kuimarisha taifa,” Rais Kenyatta akarai Wakenya.

Kenya imethibitisha zaidi ya wagonjwa 200, kwa muda wa saa 24 zilizopita watu tisa zaidi wakipatikana na virusi hivyo jumla idadi ya wenye Covid – 19 nchini ikifikia 234. Waliofariki kutokana na virusi hivyo kufikia Alhamisi walikuwa 11, 53 wakitangazwa kupona kabisa.