Habari za Kitaifa

Tutatuma vijana milioni moja ng’ambo mwaka huu – Moses Kuria

January 23rd, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KENYA itawapeleka jumla ya vijana milioni moja kupata ajira katika mataifa ya nje mwaka huu, baada ya kubuni mwafaka na mataifa kadhaa.

Kulingana na Waziri wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria, Kenya tayari imebuni utaratibu kuhusu vile vijana hao watasafiri katika mataifa hayo kuanzia mwezi huu.

Baadhi ya nchi ambazo Kenya imebuni makubaliano nazo ni Israeli, Qatar, Milki ya Kiarabu (UAE), Saudi Arabia, Canada, Ujerumani na Australia.

Mnamo Jumapili, Bw Kuria alisema kuwa Kenya na Israeli zishabuni mwafaka kuwasafirisha vijana wapatao 140,000 kufanya kazi za ujenzi katika taifa hilo.

“Majuzi, nilimaliza mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Israeli kuhusu idadi ya nafasi za kazi zilizopo na wakati vijana hao watasafiri katika nchi hiyo kuchukua kazi hizo,” akasema Bw Kuria, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni.

Waziri alisema kuwa mpango huo ni sehemu mikakati inayoendeshwa na serikali ya Kenya Kwanza kukabili kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini.

Kulingana na Bw Kuria, nafasi hizo zitawalenga vijana wanaofuzu kutoka Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS), kwani wengi wao wana ujuzi wa kiufundi unaohitajika katika mataifa hayo.

“Ikizingatiwa kuwa hili litatuhitaji tutoe stakabadhi nyingi za usafiri kama vile paspoti, tunaweka mikakati kuanzisha vituo vya kutoa paspoti karibu na mashirika ya NYS, kwa mfano lile lililo eneo la Ruaraka, jijini Nairobi,” akasema Bw Kuria.

Waziri alisema kuwa vijana hao watalipwa mishahara minono, kwani wale watakaosafiri nchini Israeli watakuwa wakilipwa dola 2000 za Amerika (Sh320,000 za Kenya) kila mwezi.

“Sijakuwa nchini kwa muda. Nilikuwa nimesafiri katika nchi hizo kubuni mkakati kuhusu vile vijana hao watasafiri katika mataifa hayo. Mnamo Machi, nitaelekea katika nchi za Ujerumani na Canada kumaliza makubaliano hayo,” akasema.

Kulingana na waziri, kando na vijana watakaochukuliwa kutoka NYS, kutakuwa na zoezi la kuwachukua vijana wengine kutoka kila eneobunge.

Bw Kuria alisema serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa shughuli za kuwachukua vijana hao zitaendeshwa kwa uwazi.

Alisema kuwa makubaliano hayo ni kati ya serikali ya Kenya na mataifa husika, hivyo vijana hao hawatatakiwa kulipa fedha zozote.