Michezo

Tutawakabili wapinzani vilivyo – Mbotela Kamaliza

June 15th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Mbotela Kamaliza ni miongoni mwa vikosi vinavyoshiriki mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu huu.

Wachezaji hao wanaamini kuwa wanatosha mboga kuvuruga wapinzani wao na kumaliza kati ya nafasi bora katika jedwali la kipute hicho muhula huu.

Licha ya kupata ushindani mkali kwenye kampeni za kipute hicho viongozi wake wanasema wanalenga kujitahidi kufa kupona ili wahaakikishe wamekwepa shoka la kushushwa ngazi msimu ujao.

Mbotela Kamaliza ilipandishwa ngazi kushiriki kipute hicho ilipoibuka kati ya nafasi mbili bora kwenye mechi za kuwania taji la Nairobi East Regional League (NERL) muhula uliyopita.

”Kiukweli sina shaka kupongeza vijana wangu kwa kuonyesha ukakamavu tosha na kukabili wapinzani wao kwa udi na uvumba kwenye mechi 14 ambazo tumecheza kufikia sasa,” amesema kocha wake mkuu, Eric ‘Bobby’ Otieno.

Kocha David Dinda wa Bomas of Kenya.

Mbotela Kamaliza iliyowahi shiriki ngarambe hiyo misimu iliyopita imeibuka kati ya vikosi vinavyolenga kufanya kweli kinyume na matarajio ya wengi.

Mlipuko wa virusi vya corona ulichangia shughuli za michezo kote duniani kupigwa stopu mnamo mwezi Machi. Kufikia kipindi hicho kwenye msimamo wa kipute hicho, Mbotela ilikuwa imekamata tisa bora kwa alama 18, moja mbele ya waliokuwa wapinzani wao Uprising FC.

Hata hivyo kikosi hicho kina mechi tatu kapuni za mkumbo wa kwanza ambapo kinastahili kucheza dhidi ya MKU FC, Rware FC na Tandaza FC.

Ofisa wa kiufundi, Washington Bululu anasema ”Ninaamini tumeketi pazuri kukabili wapinzani wetu na kupiga hatua kwenye jitihada zetu za kufanya kweli msimu huu.”

Vision United inayoshiriki kipute hicho.

Aliongeza kulingana na matokeo ya mechi hizo wanazidi kujihakikishoa nafasi ya kusalia kushiriki kipute hicho msimu ujao.

Anadokeza kuwa hata FKF ikiamua kumaliza kinyang’anyiro hicho kwa kutumia msimamo wa mechi za mkumbo wa kwanza wao wameketi pazuri kusalia miongoni mwa kumi bora.

Naye naibu kocha, Kelly Ametesha anasema “Tuna imani tosha kwamba tukiendelea kukaza buti michezoni tutafanya kweli mradi tucheze mechi zetu kwa umakini pia bila kuwapuuza wapinzani wetu.”

Kikosi hicho kinajivunia kunasa huduma za wachezaji kadhaa wapya. Orodha yao inajumuisha:mnyakaji Nicholas Munangwe, Michael Masaba, Dennis Mihingo, mshambWilliam Ochieng Olayo aliyetokea Naivas FC na Mark Blessed Omwoha bila kusahau straika, Oliver Mkonza.

Pia inajumuisha: Brandon Oduor, Emmanuel Atulo, Benson Kitur, Victor Odera, Vincent Chagala, Brian Ode, Vitalis Opiyo, Patrick Kadenge, Stephen Babu, Tom Odongo, Kenneth Okubasu, Patrick Opimbi na Hannington Young kati ya wengine.

Katika jedwali la mechi za kundi hilo Equity Bank FC inazidi kupepea ambapo inaongoza kwa kuzoa alama 36, tano mbele ya Tandaza FC baada ya kila moja kucheza mechi 15.

Nao wachana nyavu wa Shofco FC wamefunga tatu bora kwa kutia kapuni pointi 30 baada ya kuingia dimbani mara 16. Washiriki wengine wakiwa Alfones FC, JYSA FC, Uweza FC, Commercial FC, Wajiji FC, Dimba Patriots na Gathanga FC.